Safari ya Abbas Araqchi mjini Kabul; ushirikiano mzuri wa Iran na Afghanistan
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu anayehusika na masuala ya kisiasa amekutana na kufanya mazungumzo mjini Kabul na Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afganistan na kujadili masuala ya kupanua ushirikiano wa pande mbili katika nyanja zote
Abbas Araqchi, alasiri ya Jumatano ya jana aliwasili huko Kabul. Mazungumzo kuhusiana na hati jumuishi ya ushirikiano wa Iran na Afghanistan ndilo lengo kuu la safari ya Abbas Araqchi nchini Afghanistan. Hati hiyo jumuishi ni ya ushirikiano wa nyanja zote zikiwemo sekta za kiuchumi, kisiasa, wakimbizi na kuingia na kutoka Waafghani katika mipaka ya pamoja ya nchi mbiliz hizi.
Katika uwanja huo, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu anayehusika na masuala ya kisiasa amesema katika mazungumzo yake na Muhammad Hnif Atmar, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan kwamba, Tehran iko tayari kustawisha uhusiano wake na Kabul katika nyanja zote.
Kwa upande wake Muhammad Hanif Atmar, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan ameashiria uhusiano imara wa nchi mbili hizo na kueleza kuwa, kustawishwa ushirikiano wa Iran na Afghanistan na kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa hapo kabla ni jambo muhimu na la dharura.
Safari ya Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu anayehusika na masuala ya kisiasa huko Kabul inafuatia safari ya hivi karibuni ya mwishoni mwa mwezi uliopita wa Juni ya Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan hapa Tehran jambo ambalo linaonyesha kuweko azma na irada ya kweli ya nchi mbili hizi ya kuimarisha ushirikiano wao.
Iran na Afghanistan zikiwa nchi mbili jirani na kubwa zaidi zikiwa na mashirikiano mengi ya pamoja kama ya kiutamaduni, kidini na kilugha zina fursa nzuri za kupanua ushirikiano wao ambapo chimbuko la ushirikiano wa namna hii ni wananchi na mahusiano ya kirafiki baina ya nchi mbili. Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Iran imekuwa mwenyeji bora na mwema wa wakimbizi wa Kiafghani na maisha yao ya muda mrefu hapa nchini ni ishara ya wazi juu ya kuwa imara na madhubuti uhusiano wa nchi mbili hizi jirani zenye na utamaduni na ustaarbu mkongwe wa pamoja.
Kupatiwa wakimbizi wa Kiafghani huduma na suhula kama za kitiba, masomo na kadhalika hapa Iran ni dhihirisho la wazi la mtazamo wa kiutu na kibinadamu iliyonayo Tehran kwa Kabul. Kiwango hiki cha ushirikiano wa kirafiki sababu yake ni kuweko miziz imara ya mambo mengi ya pamoja ya mataifa haya mawili. Katika mazingira kama haya, kufanyika juhudi za kupanua na kustawisha zaidi ushirikiano huu ndio mambo ambayo yamewekwa katika ajenda za serikali za Tehran na Kabul.
Mazungumzo endelevu yenye lengo ya kutafuta Ramani ya Njia kwa shabaha ya kuainisha fremu ya ushirikiano jumuishi na wa muda mrefu ndilo takwa la Iran na Afghanistan ambalo lilizingatiwa na kutiliwa mkazo katika safari ya Muhammad Hanif Atmar hapa Tehran na safari ya sasa ya Abbas Araqchi huko Kabul.
Mazungumzo ya Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afganistan hapa mjini Tehran mwishoni mwa mwezi uliopita wa Juni yalifanyika katika wakati mwafaka sambamba na wimbi la vyombo maalumu vya habari la kutia matole uhusiano wa Iran na Afghanistan ambapo mwisho wa mazungumzo hayo, pande mbili zilifikia makubaliano kwamba, katika kipindi cha miezi mitatu ijayo zipasishe katika hatua ya mwisho hati jumuishi ya ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Kuhusiana na hilo, Ali Rabiei msemaji wa serikali ya Iran aliitathmini safari ya Muhammad Hanif Atmar, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan hapa Tehan kwamba, ilikuwa chanya na kusema: Matunda muhimu kabisa ya safari hiyo ni makubaliano ya nchi mbili ya kutiliana saini hati jumuishi ya ushirikiano wa pamoja.
Kuzingatiwa mambo ya pamoja ya Iran na Afghanistan kumepelekea kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hizi jirani na rafiki. Fauka ya hayo, kupatikana amani na uthabiti nchini Afghanistan ni jambo muhimu mno kwa Iran, kwani usalama wa jirani yake wa mashairiki ni usalama wake pia. Iran sambamba na kufanya mazungumzo ya kustawisha zaidi uhusiano na Afghanistan, imefuatilia pia mazungumzo ya kieneo na kimataifa kwa ajili ya kupatikana amani na usalama nchini Afghanistan ambapo hadi sasa hilo limekuwa na mafanikio ya kuridhisha.