Iran: Makombora yetu yana uwezo na muundo wa kipekee
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63177-iran_makombora_yetu_yana_uwezo_na_muundo_wa_kipekee
Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema makombora yaliyozalishwa hapa nchini yana muundo wa aina yake na uwezo wa kipekee, jambo ambalo limeimarisha uwezo wa kujihami taifa hili.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 02, 2020 08:02 UTC
  • Iran: Makombora yetu yana uwezo na muundo wa kipekee

Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema makombora yaliyozalishwa hapa nchini yana muundo wa aina yake na uwezo wa kipekee, jambo ambalo limeimarisha uwezo wa kujihami taifa hili.

Brigedia Jenerali Kioumars Heidari alisema hayo jana katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim na kuongeza kuwa, Iran imeunda aina kadhaa za zana za kijeshi ili kukidhi mahitaji yake ya kiulinzi.

Amebainisha kuwa, makombora ya Jamhuri ya Kiislamu yana sifa za kipekee na yameundwa na wataalamu wa humu kwa namna kwamba yana uwezo wa kulenga shabaha kwa usahihi mkubwa. 

Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mambo mengine yanayofanya makombora ya taifa hili yawe ya kipekee ni namna yalivyo erevu na ya kiotomatiki.

Brigedia Jenerali Kioumars Heidari

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jeshi la Iran lilizindua aina mbili za makombora ya balestiki na cruise wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ulinzi. Katika uzinduzi huo, Jamhuri ya Kiislamu iliweka hadharani kwa mara ya kwanza kombora la balestiki liitwalo Shahidi Qassem Soleimani na kombora la cruise lililopewa jina la Shahidi Abu Muhandis.

Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya ulinzi huku ikijitosheleza kwa kiasi kikubwa katika zana za kujihami. Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa, uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi zingine bali sera yake ya ulinzi imejengeka katika msingi wa kujihami.