Sep 11, 2020 07:42 UTC
  • Maqarii wa Qurani wa Ulimwengu wa Kiislamu walaani kuvunjiwa heshima Mtume SAW

Maqarii mashuhuri wa Qurani Tukufu kutoka kona mbalimbali za dunia wamekutana mjini Mashhad, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo kwa kauli moja, wamelaani vikali hatua ya jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo ya kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW.

Wasomaji hao bingwa wa Qurani Tukufu, wa kike na kiume wanatoka katika nchi za Iran, Pakistan, Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, India, Bangladesh, Sierra Leone, Nigeria, Burkina Faso, Iraq, Lebanon, na Syria.

Taarifa ya mwisho ya maqarii hao baada ya mkutano wa mji mtakatifu wa Mashhad imesema: Taasisi za ulimwengu wa Kiislamu zinalaani kitendo cha jarida la Charlie Hebdo cha kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW, na kuitaka jamii ya kimataifa kuwashughulikia vilivyo wanaotusi matukufu ya dini za Mbinguni.

Taarifa hiyo ya wasomi mashuhuri wa Qurani Tukufu duniani imeongeza kuwa, kudhalilishwa Mtume wa Uislamu ni kitendo cha kihaini na kisichovumilika.

Maandamano ya kulaani vikali kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW mjini Tehran

Jana Alkhamisi, wananchi wa Iran katika kona zote za nchi waliandamana kuonesha kukasirishwa mno na hatua ya jarida ya Charlie Hebdo la Ufaransa wa kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na pia kitendo cha maadui wa Uslamu cha kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu katika mji wa Malmö wa kusini mwa Sweden.

Aidha maandamano ya kulaani vikali kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW yanaendelea kufanyika hapa nchini hii leo kwa siku ya pili mfululizo, huku waandamanaji hao wakisisitiza kuwa, vitendo hivyo viovu na vya kifidhuli vya maadui wa Uislamu barani Ulaya vinapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote.

 

Tags