Khatibzadeh: Vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vitaondolewa tarehe 18 Oktoba
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran unatarajiwa kumalizika usiku wa tarehe 18 mwezi huu.
Saeed Khatibzadeh amesema hayo jana katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari na kueleza kwamba, tarehe 18 mwezi huu itakuwa siku nyingine ya kushindwa Marekani; kwani muda wa vikwazo vya kuingiza na kusafirisha silaha nje ya nchi utamalizika na vilevile marufuku ya kusafiri shakhsia 23 nayo itaondolewa.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ameeleza kwamba, licha ya ukwamishaji mambo, ubabe na hatua zisizo za kisheria za Marekani, serikali ya Trump imeshindwa kusukuma mbele gurudumu la malengo yake na kwa mara nyingine tena Tehran imeonyesha kuwa, kinyume na ilivyokuwa ikijitutumia kumbe Washington haina ubavu na nguvu kiasi hicho.
Itakumbukwa kuwa, moja kati ya vipengee muhimu vya mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lina kipengee kuhusu kufutwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran miaka mitano baada ya kuanza kutekelezwa mapatano hayo.
Baada ya kupitishwa azimio 2231 la Baraza la Usalama mwaka 2015, Iran ilipigwa marufuku kununua au kuuza zana aina saba za kivita ikiwa ni pamoja na vifaru, magari ya deraya, mizinga, ndege za kivita, helikopta, manoari na makombora.
Vikwazo hivyo vya silaha dhidi ya Iran vinatazamiwa kuondolewa Oktoba 18 mwezi huu ambapo licha ya njama zake za kila upande, Marekani imeshindwa kutekeleza madi yake kwamba, itahakikisha muda wa vikwazo hivyo dhidi ya Iran unaongezwa.