Sera za upande mmoja za Marekani ni tishio kwa jamii ya kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64038-sera_za_upande_mmoja_za_marekani_ni_tishio_kwa_jamii_ya_kimataifa
Mjumbe wa Iran katika Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema kuendelea sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ni tishio la kimataifa katika kuunga mkono na kuinua kiwango cha haki za binadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2020 23:05 UTC
  • Sera za upande mmoja za Marekani ni tishio kwa jamii ya kimataifa

Mjumbe wa Iran katika Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema kuendelea sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ni tishio la kimataifa katika kuunga mkono na kuinua kiwango cha haki za binadamu.

Mohammad Zareian aliyasema hayo Jumatano katika kikao cha Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa: “Hatua za upande mmoja na zenye taathira mbaya na zilizo  kinyume cha sheria, ambazo zimelazimishwa kwa watu wa Iran, zimeshadidishwa hata wakati huu wa janga la corona.”

Sera za utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya taifa la Iran ni kilele cha dhihirisho la kujichukulia maamuzi ya upande mmoja katika uga wa kimataifa. Sera hizo mbali na kuwa zinakiuka haki za kimsingi za watu wa Iran pia ni tishio kwa usalama wa dunia.

Baada ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018, ilichukua uamuzi wa kuiwekea Iran vikwazo shadidi zaidi vya kiuchumi. Vikwazo hivyo vimeshadidishwa zaidi katika kipindi hiki cha janga la corona.

Vikwazo vipya dhidi ya benki 18 za Iran, kuzuia dawa za magonjwa maalumu kuingia Iran, kuzuia kuingia Iran dozi milioni mbili za chanjo ya influenza ambayo ilikuwa imeagizwa na Hilali Nyekundu ya Iran, na vikwazo vya kiuchumi, yote hayo ni katika fremu ya sera za Marekani za  kulinyima taifa la Iran haki zake na bila shaka hatua kama hiyo ni ugaidi wa kiuchumi.

Kuhusiana na nukta hii, Ismail Baghaei Hamaneh, mwakilishi wa Iran katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa mjini Geneva amesema, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani ni jinai dhidi ya binadamu na kukosoa sera za Ulaya za kukaa kimya mbele ya sera za Marekani za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja.

Hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha kimya cha jamii ya kimataifa hasa Ulaya mbele ya hatua za Marekani za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kuwazuia watu wa Iran kufikia maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi. Kunyamazia kimya sera hizo haribifu za Marekani ni jambo ambalo linaweza kuhatarisha maslahi ya jamii ya kimataifa.

Kutumia sera za mabavu katika kuyanyima mataifa ya dunia haki za kimsingi za maisha ni ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu. Aidha kupuuza misingi ya haki za binadamu katika kuondoa vikwazo ni ukiukwaji wa wazi wa kanuni za kimataifa.

Kuheshimu na kuzingatia misingi ya kimataifa ni nukta ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na amani na usalama wa dunia na kwa hivyo inatarajiwa kuwa jamii ya kimataifa haitanyamazia kimya sera za Marekani za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja.

Kuhusiana na hili, Mohsen Baharvand, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kimataifa anaamini kuwa, nchi za dunia zinapaswa kupinga sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja kwa kuungana na kupaza sauti moja.

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu

Pamoja na hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama nchi huru, imekuwa ikitetea haki za watu wake mkabala na hatua haribifu za Marekani kwa kuwasilisha malalamiko kupitia taasisi za kimataifa. Kwa mfano, Iran imewasilisha malalamiko yake mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) kuhusu vikwazo vya Marekani dhidi ya watu wa Iran.

Mbali na hayo, Idara ya Haki za Binadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapanga kuwasilisha mashtaka dhidi ya watu  45 wa Marekani ambao wamehusika katika kuwawekea wananchi wa Iran vikwazo vya kidhalimu.

Kama alivyosema Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, utawala wa Marekani unabeba dhima ya kufidia hasara iliyopatikana kutokana na vikwazo vyake dhidi ya taifa la Iran.