Wanasayansi wa Iran wako imara kukabiliana na ubeberu wa Marekani
Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran imetangaza kuwa, wanasayansi na wasomi wa Iran wako imara katika kukabiliana na ubeberu na uistikbari wa Marekani kwenye nishati ya nyuklia.
Taarifa ya jana Alkhamisi ya taasisi hiyo imetoa tamko hilo kujibu upayukaji mpya wa Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani kuhusu kustafidi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nishati ya nyuklia.
Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran imesema, wasomi wa sekta ya nyuklia wa Iran wanafuata miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na wako imara na tayari muda wote kupambana na uistikbari wa serikali ya Marekani katika suala zima la nishati ya nyuklia.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kuangalia mbele katika matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia ndio msingi wa kiistratijia wa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba taifa la Iran litaendelea daima kuwa na nguvu hizo za nyuklia za matumizi ya kiraia.
Katika madai yake ya hivi karibuni kabisa, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo, amedai kuwa, Iran inasema haitaki silaha za nyuklia lakini inautishia ulimwengu kwa mradi wake wa nyuklia, hivyo mataifa yote ya dunia yanapaswa kusimama kidete kukabiliana na Iran.
Upayukaji huo wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani unashuhudiwa katika hali ambayo dunia nzima inaelewa kuwa hata Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umethibitisha kimaandishi mara chungu nzima kwamba mradi wa nyuklia wa Iran ni wa amani kikamilfu, si wa silaha za atomiki na hauna madhara yoyote duniani.