Iran yazindua mfumo mpya wa kuvurumisha makombora ya balestiki
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC limezindua mfumo erevu na wa kiotomatiki wa kuvurumisha makombora kadhaa ya balestiki ya masafa marefu kwa wakati mmoja.
Mfumo huo wa makombora ulioundwa na wataalamu wa humu nchini wa Kikosi cha Anga za Mbali cha IRGC, umezinduliwa hii leo na Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH).
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Meja Jenerali Salami amesema: Uzinduzi wa makombora yetu unawatia kiwewe maadui. Uwezo wetu wa makombora ni dhamana ya kuondoka maadui.
Amesema uwezo mkubwa wa kiulinzi na kujihami wa Jamhuri ya Kiislamu unalipa taifa hili nguvu za kuonyesha irada yake ya kisiasa, na nguvu zake zinazoweza kutumika dhidi ya adui iwapo italazimu.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya ulinzi huku ikijitosheleza kwa kiasi kikubwa katika zana za kujihami.
Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa, uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi zingine bali sera yake ya ulinzi imejengeka katika msingi wa kujihami.