Meja Jenerali Salami: Tutalipiza kisasi cha damu ya kamanda Suleimani kwa waliomuua
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesisitiza tena akisema: "Tutalipiza kisasi cha damu ya kamanda shahidi Qassim Suleimani kwa waliomuua."
Meja Jenerali Hussein Salami ameyasema hayo mjini Tehran katika mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Iraq Juma Anad Saadoun, ambapo mbali na kusisitiza kuwa ulipizaji kisasi huo hauna uhusiano wowote na ufuatuliaji wa mchakato wa kisheria wa kuuliwa shahidi kamanda Qassim Suleimani na Abu Mahdi al Muhandis, amesema ana matumaini kizazi cha Wairaq nacho pia kitalipiza kisasi cha damu ya kamanda wake shujaa, shahidi Abu Mahdi al Muhandis.
Meja Jenerali Salami ameongeza kuwa, hapana shaka yoyote kuwa katika Ulimwengu wa Kiislamu kamanda Qassim Suleimani na Abu Mahdi al Muhandis ndio waliotoa mchango mkubwa kabisa uliowezesha kusambaratishwa na kuangushwa DAESH(ISIS) na mipango ya Kizayuni na Kimarekani katika eneo.
Sambambana na kuashiria kuwa matamanio ya Iran kwa Iraq ni kuona nchi hiyo inakuwa huru, iliyojitawala, iliyoungana pamoja na yenye nguvu na amani, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo pia ulazima kuondoka au kutimuliwa jeshi vamizi la kigaidi la Marekani katika ardhi ya nchi hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Iraq Luteni Jenerali Juma Anad Saadoun amesema, Iran iliipatia misaada muhimu sana Iraq katika kipindi hasasi cha hujuma na uvamizi wa Daesh.
Anad Saadoun ameongeza kuwa: "ndugu zetu wa Iran walitusaidia katika kupambana na ugaidi wa Daesh na walitupatia kila tulichohitaji katika kipindi kile; na sisi hatutalisahau jambo hili".../