Dec 24, 2020 08:16 UTC
  • Zarif amshambulia Trump kwa kuihusisha Iran na mashambulio ya Iraq

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemjia juu Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ameituhumu Tehran kuwa imehusika na mashambulio ya maroketi dhidi ya ubalozi wa US mjini Baghdad, Iraq.

Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter leo Alkhamisi, Mohammad Javad Zarif amemhutubu Trump kwa kumuambia kuwa, kuyaweka hatarini maisha ya Wamarekani katika nchi ajinabi hakutopotosha fikra za walio wengi juu ya kufeli kwake ndani ya Marekani.

Ujumbe huo wa Twitter wa Zarif umeambatanishwa na jumbe kadhaa za miaka ya huko nyuma ya Trump, ukiwemo wa mwaka 2011 ambapo alimshambulia vikali mtangulizi wake Barack Obama akimtuhumu kuwa alitaka kutumia vita kama wenzo wa kutaka kuchaguliwa tena.

Dakta Zarif pia ameambatanisha ujumbe wa Twitter wa Trump wa mwaka 2012 alipodai kuwa, "daima nimekuwa nikisema kuwa Barack Obama ataishambulia Iran katika hali fulani kabla ya uchaguzi."

Ujumbe wa Twitter wa Dkt Zarif

Huku akipuuza tahadhari zake alizotoa huko nyuma dhidi ya Obama akimtuhumu kuwa ni mpenda vita, Trump jana Jumatano pasina kutoa ushahidi wowote alidai kuwa: Iran imehusika na mashambulio ya maroketi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad siku ya Jumapili.

Katika ujumbe huo wa kifidhuli, Trump kwa jeuri aliandika kuwa: Ushauri wa kirafiki kwa Iran, iwapo Mmarekani mmoja atauawa (katika mashambulio hayo), basi nitaibebesha dhima Iran. Tafakari juu ya hilo.

Wakati huohuo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh sambamba na kupuuzilia mbali madai hayo yasiyo na msingi ya Trump dhidi ya Iran, ameonya kuwa, hatua yoyote ya kichokozi na isiyo na mantiki ya Marekani itapata jibu mwafaka.

Tags