Jan 13, 2021 08:12 UTC
  • Iran yailaani Marekani kwa kuiweka Cuba katika orodha ya 'waungaji mkono ugaidi'

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hatua ya Marekani kuiweka Cuba katika orodha ya nchi ambazo eti zinaunga mkono ugaidi. Iran aidha imesema inafungamana na Cuba katika mapamano yake dhidi ya madola ya kibeberu duniani.

Katika taarifa siku ya Jumanne, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hakuna nchi yoyote, hasa Marekani, yenye haki ya kuingilia mambo ya ndani ya Cuba au kuiamulia iwe na uhusiano na nchi gani.

Amesema utawala wa kigaidi wa Marekani unapaswa kukumbushwa kuwa, Cuba ni mwanachama amilifu wa Umoja wa Mataifa na nchi hiyo ilikuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza yaliyobeba bendera ya kupambana na ubeberu  pamoja na uistikbari wa kimataifa. Aidha amesema Iran inapinga vikali hatua hiyo ya utawala wa kigaidi wa Marekani na kuongeza kuwa Washington imekuwa na misimamo ya kindumakuwili kwani ilimuua kigaidi Shahidi Qassem Soleimani sambamba na kuunga mkono makundi ya kigaidi kama vile ISIS au Daesh. 

Amesema Iran itaendelea kuiunga mkono Cuba kikamilifu na itaimarisha uhusiano wake na nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodríguez Parrilla

Katika hali ambayo utawala wa Rais Barack Obama uliiondoa Cuba katika orodha ya nchi zinazodaiwa kuunga mkono ugaidi, utawala wa Donald Trump ambao uko katika siku zake za mwisho umebatilisha uamuzi huo.

Utawala wa Trump haujatoa ushahidi wowote wa kuthibitisha madai yasiyo na msingi kuwa eti Cuba inaunga mkono ugaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodríguez Parrilla amelaani vikali hatua hiyo ya Trump na kuitaja kuwa ya kinafiki. Amesema wale wote wanaopambana kiukweli na ugaidi wanafahamu uamuzi huo wa utawala wa Trump ni wa kisiasa na usio na mashiko.

 

 

Tags