Feb 20, 2021 03:06 UTC
  • Chanjo ya Corona ya Sputnik V ya Russia kuanza kutegenezwa Iran

Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa, chanjo ya Corona au COVID-19 ya Sputnik V ya Russia sasa itaanza kutengenezwa hapa nchini.

Akizungumza na Shirika la Habari la IRNA, Mahmoud Vaezi, Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Iran amesema sasa mbali na kuwa Iran inanunua moja kwa moja chanjo ya Sputnik V kutoka Russia chanjo hiyo pia itaanza kutegenezwa hapa nchini kufuatia mapatano yaliyofikiwa baina ya nchi hizo mbili.

Aidha amedokeza kuwa, Taasisi ya Pasteur ya Iran inashirikiana na Cuba katika kutengeneza chanjo ambayo imeshafanyiwa majaribio ambayo nayo pia itaanza kuzalishwa ndani ya Iran.

Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Iran ameongeza kuwa, Iran pia imeagiza dozi 250,000 za chanjo ya Corona kutoka China na halikadhalika inatarajia pia kununua chanjo zingine kutoka India na Sweden.

Aidha Iran inaendelea na majaribio ya chanjo ya Corona iliyotengenezwa na wanasayansi Wairani ijulikanayo kama COVIRAN Barekat. Chanjo hiyo imeshafanyiwa majaribio yaliyofana kwa wanadamu na inatarajiwa kuanza kutegenezwa kwa wingi baada ya muda usio mrefu.

Shehena ya chanjo ya Sputnik ikiwasili mjini Tehran

Iran iko mbioni kutengeneza chanjo zingine za corona ndani ya nchi na pia kwa ushirikiano na washirika wa kigeni.

Hivi karibuni, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizindua mpango wa kitaifa wa chanjo ya Corona. Rais alimpongeza Waziri wa Afya Daktari Saeed Namaki kwa kumdunga mwanae wa kiume chanjo ya kwanza kabisa katika hatua ya kujenga imani miongoni mwa wananchi kuhusu chanjo hiyo.

Waziri wa Afya Daktari Namaki amesema wafanyakazi wa hospitali 635 za kiserikali na za sekta binafsi nchini ambazo zinawahudumia wagonjwa wa corona watapata chanjo hiyo.

Amesema awamu ya pili ya chanjo ya corona itaanza kwa kuwalenga wale wenye magonjwa sugu na wazee na kisha baada ya hapo wananchi wengine wa kawaida watachanjwa.

Tags