Takht-Ravanchi: Vikwazo vinashadidisha matatizo katika mabadiliko ya tabianchi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i67200-takht_ravanchi_vikwazo_vinashadidisha_matatizo_katika_mabadiliko_ya_tabianchi
Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, vikwazo vya kiuchumi vya upande mmoja ni moja ya vizuizi vikuu vinavyokwamisha juhudi za kukabiliana ipasavyo na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, hivyo lazima viondolewe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 23, 2021 23:45 UTC
  • Takht-Ravanchi: Vikwazo vinashadidisha matatizo katika mabadiliko ya tabianchi

Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, vikwazo vya kiuchumi vya upande mmoja ni moja ya vizuizi vikuu vinavyokwamisha juhudi za kukabiliana ipasavyo na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, hivyo lazima viondolewe.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Majid Takht-Ravanchi akisema hayo jana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kwa ajili ya kuchunguza athari mbaya za kiusalama za mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema, ili kuweza kukabiliana vilivyo na athari mbaya za vikwazo vya upande mmoja kwa mazingira na hali ya hewa, inabidi kuchukuliwe hatua za pamoja na kwamba tawala zote duniani zinapaswa kuheshimu na kutekeleza kikamilifu ahadi zao ndani ya Mkataba wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Makubaliano ya Paris.

Nchi za viwanda ndio wahatarishaji wakubwa wakubwa wa usalama wa mazingira na tabia nchi duniani

 

Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, vikwazo vinadhoofisha vibaya uwezo wa nchi nyingi zinazoendelea duniani ikiwemo Iran katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran si tu ni kizuizi cha kuweza Tehran kupata vyanzo vya fedha na teknolojia inayotakiwa, lakini pia vinaikwamisha Iran kutumia uwezo wake wa ndani katika kutekeleza ahadi zake kwa namna inayotakiwa, hivyo vikwazo hivyo haramu na visivyo vya kibinadamu, lazima viondolewe.

Amesema, ni ukweli usiopingika kwamba, sababu nyingi kuu na za kimsingi zinazohatarisha usalama wa mazingira na hali ya hewa duniani hususan barani Afrika, hazisababishwi na nchi za maeneo hayo, bali nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani, ndio wahatarishaji wakuu wa usalama wa mazingira na hali ya hewa ulimwenguni.