Mar 07, 2021 08:01 UTC
  • Iran kujenga bandari kubwa zaidi ya kibiashara katika Bahari ya Oman

Mkurugenzi Mwandamizi wa Shirika la Bandari na Ubaharia la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza habari ya kujengwa bandari kubwa zaidi ya kibiashara ya Iran katika Bahari ya Oman na katika eneo la Kuhe Mubarak katika wilaya ya Jask katika mkoa wa Hormozgan, kusini mwa nchi.

Akifafanua suala hilo, Muhammad Rastad, Mkurugenzi Mwandamizi wa Shirika la Bandari na Ubaharia la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa bandari hiyo kubwa ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba meli kubwa zaidi duniani itajengwa katika ufukwe wa Makran, na kuwa ujenzi huo utatekelezwa katika hatua tatu tofauti. Ameongeza kuwa bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba uzani wa tani milioni 100 hadi 200.

 

Muhammad Rastad amesema kwamba kwa kutilia maanani kuwa meli za mizigo ndizo zilizo na mchango mkubwa katika sekta ya biashara baharini katika ulimwengu wa sasa, uamuzi wa Iran wa kujenga bandari hiyo nje ya Lango Bahari la Hormoz itaikaribisha zaidi na njia kuu ya biashara ya kimataifa na hivyo kuzikurubisha zaidi kibiashara nchi za Mashariki na Magharibi.

Kuhe Mubarak ni moja ya wilaya za mkoa wa Hormozgan uliopo kusini mwa Iran na ipo katika eneo la jangwani katika ufukwe wa Bahari ya Oman.

Tags