Apr 13, 2021 07:54 UTC
  • Chanjo ya Corona ya Barekat kuanza kuzalishwa kwa wingi nchini Iran wiki ijayo

Mwenyekiti wa Ofisi Kuu ya Kutekeleza Maagizo ya Imam Khomeini amesema Wakfu wa Barekat wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utaanza kuzalisha kwa wingi chanjo ya kukabiliana na virusi vya Corona ya 'COVIran Barekat' kuanzia wiki ijayo Aprili 21.

Akizungumza na shirika la habari la IRNA, Mohammad Mokhber amesema ameridhishwa mno na mchakato wa uzalishaji kwa wingi wa chanjo hiyo ya kupambana na ugonjwa wa Covid-19 hapa nchini.

Mokhber amebainisha kuwa, mchakato wa kuandaa mazingira ya kuzalisha dozi milioni tatu katika awamu ya kwanza ya uzalishaji huo umekamilika. Ameongeza kuwa, Wakfu wa Barekat unajiandaa kuzalisha dozi milioni 12 katika awamu ya pili ya uzalishaji huo.

Iran imesema karibuni itakuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa chanjo ya Corona

Mwenyekiti wa Ofisi Kuu ya Kutekeleza Maagizo ya Imam Khomeini amesema anatumai kuwa, kampeni ya uchanjaji wa umma kwa chanjo hiyo iliyozalishwa hapa nchini itaanza mwezi wa tatu wa Kiirani wa Khordad, unaoanza Mei 22.

Iran iko mbioni kuunda chanjo kadhaa za Covid-19, ambapo mbali na  chanjo ya hiyo COVIran Barekat, chanjo zingine ambazo zimepiga hatua nzuri katika majaribio ni pamoja na Razi Cov Pars,  Fakhra na chanjo ya pamoja ya Taasisi ya Chanjo ya Finlay ya Cuba na Taasisi ya Chanjo ya Pasteur ya Iran.

 

Tags