Iran: Kurutubisha urani kwa 60% ni jibu kwa njama za maadui
(last modified Mon, 19 Apr 2021 02:54:14 GMT )
Apr 19, 2021 02:54 UTC
  • Iran: Kurutubisha urani kwa 60% ni jibu kwa njama za maadui

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema urutubishaji wa madini ya urani kwa kiwango cha asilimia 60 hapa nchini ni jibu kwa njama na chokochoko za maadui wa taifa hili.

Akihutubia kikao cha wazi cha Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amesema hatua ya Iran kurutubisha urani kwa kiwango cha hadi asilimia 60 ni jibu mwafaka kwa ugaidi wa kinyuklia ambao ulitokea hivi karibuni katika kituo cha urutubishaji urani cha Natanz, uliolenga kudhoofisha mchakato wa mazungumzo ya Kamati ya Pamoja ya makubaliano ya JCPOA huko Vienna, Austria.

Amesema maadui wa taifa la Iran wanadhani kuwa watasimamisha shughuli za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu zenye malengo ya amani, kwa kutekeleza hujuma za kigaidi. 

Jumapili iliyopita kuliripotiwa tukio katika sehemu moja ya mtandao wa kusambaza umeme katika kituo cha kurutubisha madini ya urani cha Shahid Ahmadi Roshan huko Natanz lakini kwa bahati nzuri tukio hilo halikusababisha maafa ya binadamu wala kuvuja kwa mionzi ya nyuklia.

Spika wa Bunge la Iran ameeleza bayana kuwa, urutubishaji wa madini ya urani kwa kiwango cha asilimia 60 hapa nchini ni tukio muhimu la kisayansi na kiteknolojia na ambalo limefikisha ujumbe nyeti wa kisiasa kwa maadui.

Wiki iliyopita Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran  alimuandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), ambapo mbali na kuwasilisha malalamiko rasmi kuhusu tukio la kigaidi la Natanz, alimfahamisha kuhusu mpango wa kuanza urutubishaji wa urani kwa kiwango cha asilimia 60 katika Kituo cha Nyuklia cha Shahidi Ahmadi Roshan cha Natanz. 

Tags