Apr 26, 2021 10:59 UTC
  • Namaki: Iran imepata moja ya chanjo bora zaidi za corona duniani

Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran hivi sasa imeweza kupata moja kati ya chanjo bora na yenye uwezo zaidi ya corona au COVID-19 duniani. Amesema chanjo hiyo imetengenezwa katika Taasisi ya Pasteur ya Iran.

Daktari Saeed Namaki Waziri wa Afya wa Iran ameyasema hayo leo Jumatatu wakati wa kuzinduliwa awamu ya tatu ya majaribio ya kikliniki ya chanjo ya corona ambayo imeundwa kwa pamoja na Taasisi ya Pasteur ya Iran na Taasisi ya Finlay ya Cuba. Akizungumza katika sherehe iliyofanyika katika ukumbi wa Ibn Sina katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Isfahan, Daktari Namaki amesema chanjo hiyo imeundwa kwa teknolojia mpya zaidi na Iran ina fakhari kuwa miongoni mwa nchi zilizostawi katika uga huo.

Amesema wataalamu wamefanya kazi yao ya kuzalisha chanjo na sasa Iran itakuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uzalishaji wa chanjo ya corona kieneo.

Daktari Namaki amesema watu waliodungwa chanjo ya COVID-19 ya Taasisi ya Pasteur ya Iran wameonyesha dunia kuwa chanjo hii ni salama. Amesema katika majaribio ya kwanza na ya pili ya chanjo hiyo kulifanyika utafiti wa kina na imebainika kuwa chanjo hii ni nzuri sana na ni  kwa msingi huo ndio imepata idhini ya kufanyiwa majaribio katika awamu ya tatu.

Mtu aliyejitolea akidungwa chanjo ya corona iliyoundwa kwa pamoja na Taasisi ya Pasteur ya Iran na Taasisi ya Finlay ya Cuba

Aidha Waziri wa Afya amesema Iran imeweza kubuni njia bora zaidi za kisayansi za kukabiliana na corona pamoja na kuwa imekuwa chini ya mashinikizo makubwa na vikwazo.

Juzi pia Mkurugenzi wa timu ya utafiti na uzalishaji wa chanjo ya COVIRAN BAREKAT alisema kuwa, uzalishaji wa chanjo hiyo ya corona ya Kiirani uko katika hatua zake za mwisho.

Mashirika kadhaa ya Iran yako mbioni kutengeneza chanjo za corona na inatazamiwa kuwa katika kipindi cha miezi miwili ijayo chanjo hizo zitapata idhini ya kuanza kutumiwa ndani na nje ya nchi.

Tags