Iran inapanga kuwawekea vikwazo maafisa wa Umoja wa Ulaya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetayarisha orodha ya maafisa wa Umoja wa Ulaya ambao itawawekea vikwazo.
Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa tangazo hilo na kuongeza kuwa nchi za Ulaya zina misimamo ya kindumakuwili kuhusu haki za binadamu na zimekuwa zikitoa tuhuma kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran na kwa msingi huo Iran nayo itachukua hatua mkabala. Amesema nchi za Ulaya zimelifanya suala la haki za binadamu kuwa la kisiasa na zenyewe ndio wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu.
Amesema baada ya Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo maafisa wa Iran, Tehran imeamua kusitisha kwa muda mazungumzo yake na wakuu wa umoja huo. Aidha amesema Iran sasa imetayarisha orodha ya maafusa wa Ulaya ambao itawawekea vikwazo.
Khatibzadeh ameashiria taarifa kuhusu serikali ya Marekani kutoondoa vikwazo dhidi ya Iran na pia kuhusu dhamana ya kuondolewa vikwazo vyote na kusema: "Marekani inapaswa kuondoa vikwazo vyote vinavyohusiana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA."

Akijibu swali kuhusu mazungumzo ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA yanayofanyika Vienna, Khatibzadeh amesema Iran haina hamu ya kushiriki katika mazungumzo marefu kupita kiasia na pia wakati huo huo amesisitiza kuwa Iran haina haraka katika mazungumzo.
Ameendelea kusema kuwa, iwapo Iran itahisi hakuna irada ya kisiasa basi haitaendelea na mazungumzo hayo ya Vienna.