Araqchi: Majopokazi mawili ya nyuklia na uondoaji vikwazo yataanza kuandaa makubaliano
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshugulikia masuala ya kisiasa Sayyid Abbas Araqchi amesema, kuna changamoto kubwa katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna, pamoja na hayo amebainisha kuwa, majopokazi mawili ya nyuklia na uondoaji vikwazo yatahusika na uandaaji wa makubaliano.
Araqchi, ambaye ndiye anayeongoza ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya kamati ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo baada ya kikao cha kamati hiyo kilichofanyika huko Vienna na akaongeza kwamba, kuna changamoto kubwa na vipengele vigumu mno vya ufafanuzi wa masuala, ambavyo vinahitaji kubainishwa neno kwa neno na ibara kwa ibara hadi kufikia mwafaka juu yake.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran amesema mwenendo wa mazungumzo uko kwenye muelekeo sahihi na akabainisha kuwa, "tumejikita kwenye majopokazi matatu; majopokazi mawili ni ya nyuklia na uondoaji vikwazo, ambayo yatafanya kazi ya kuandaa makubaliano; na jopokazi la tatu ni lile litakaloratibu masuala kwa upana na namna ya kuzungumzia utaratibu wa kuthibitisha kama makubaliano yaliyofikiwa yametekelezwa ili tuweze kupata njia ya ufumbuzi katika upeo wa masuala makuu."
Sayyid Abbas Araqchi amesisitiza pia kuhusu msimamo wa Iran juu ya utaratibu wa mazungumzo kwa kusema: "Sisi tuna msingi wetu wa kwamba, hatuharakishi mazungumzo, wala hatufanyi papara na pia haturuhusu mazungumzo yawe ya urefushaji majadiliano."
Duru ya kwanza ya kamati ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ilifanyika jana jioni huko mjini Vienna, Austria kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa Iran, nchi za kundi la 4+1 na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya.../