Vaezi: Mazungumzo ya JCPOA mjini Vienna ni magumu lakini chanya
Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mazungumzo ya mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama JCPOA yanayoendelea Vienna Austria ni chanya na ya kurudhisha lakini ni magumu.
Akizungumza Ijumaa, Vaezi amesema mazungumzo hayo yanapitia kipindi muhimu sana na ingawa ni magumu lakini yanafanyika katika mazingira chanya. Amesema mkondo ukiendelea hivi kama ulivyo basi hatua zitapigwa Vienna. Aidha amesema timu ya mazungumzo ya Iran huko Vienna inazingatia masharti yaliyowekwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa msingi huo Iran inataka kuhuisha mapatano ya JCPOA na kuhakikisha kuwa vikwazo dhidi yake vinaondolewa.
Katika fremu ya utekelezaji wa hatua za kistratijia kwa ajili ya kufuta vikwazo vya kidhalimu na kulinda maslahi ya taifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilichukua hatua za kulipiza kisasi ikijibu hatua ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na vilevile hatua ya nchi za Ulaya ya kutotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Sambamba na hayo, lengo kuu la Iran ni kulindwa makubaliano hayo kama waraka wa kujenga hali ya kuaminiana. Kwa msingi huo, hivi sasa kunafanyika kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA katika ngazi ya wakurugenzi na manaibu mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na nchi wanachama katika kundi la 4+1 huko Vienna nchini Austria.
Ratiba na malengo ya mazungumzo hayo ya Vienna yako wazi. Vikwazo vyote vya Marekani vinapaswa kuondolewa, na baada ya kujihakikishia kwamba suala hilo limefanyika, Iran itasitisha hatua zake za kulipiza kisasi na kutekeleza tena vipengee vyote vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Kwingineko katika matamshi yake, Vaezi amesema Iran iko tayari kuimarisha ushirikiano na Saudi Arabia. Amesema ushirikiano wa nchi hizi mbili bila shaka ni kwa maslahi ya eneo.