Kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA kinaendelea tena Vienna Austria
Kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kinafanyika tena leo huko Vienna Austria.
Kikao hicho kinahudhuriwa na ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wawakilishi wa kundi la 1+4 ambalo linaundwa na nchi za Ujerumani, Ufaransa, Russia, China na Uingereza.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, miongoni mwa yatakayojadiliwa leo ni pamoja na kutathmini na kufikia natija jumla majopokazi matatu ya nyuklia kuhusu vikwazo na namna ya kuzungumzia utaratibu wa kuthibitisha kama makubaliano yaliyofikiwa yametekelezwa.
Baadhi ya duru zinasema kuwa, licha ya kuwa mazungumzo hayo ni magumu lakini kumepigwa hatua nzuri na kwamba, pande husika zimo katika hatua ya kuandaa muswada wa mapatano.
Timu za mazungumzo hayo pamoja na majopokazi yake yamekuwa na vikao nyeti na vigumu hivi karibuni yakijadili matini za masuala muhimu; na kikao cha leo ni mwendelezo wa vikao hivyo ambavyo lengo lake ni kujaribu kuyaokoa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hususan kadhia ya kuondolewa vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hivi majuzi Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshugulikia masuala ya kisiasa na mkuu wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya kamati ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA alinukuliwa akisema, vikwazo vyote vilivyowekwa na Marekani baada ya kusainiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, sawa viwe vimewekwa katika kipindi cha utawala wa Barack Obama au kipindi cha utawala wa Donald Trump vinapaswa kuondolewa.