Kamanda wa IRGC: Tuna furaha kuona Marekani imekasirishwa na Hashd al Sha'abi
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hossein Salami amekutana na Faleh al-Fayyad mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq maarufu kama Hashd al Sha'abi na kusema kushiriki rais wa Iraq na mkuu wa Hashd al Sha'abi katika sherehe za kuapishwa rais wa Iran ni nukta yenye ujumbe muhimu.
Salami ameongeza kuwa: "Leo tunazungumza kuhusu kuporomoka Marekani, na sehemu kubwa ya kuporomoka huko imejiri Iraq. Mapambano ya Wairaqi yameidhoofisha Marekani na kuongeza gharama zao." Akimhutubu kamanda wa Hashd al Sha'abi amesema: "Wakati tulipoona Marekani imekasirishwa na harakati zenu tulifurahi kwani ilitubainikia kuwa mnafanya kazi nzuri."
Salami amesisitiza kuwa: "Tutaendelea kuwaunga mkoono katika muendelezo wa mapambano hayo makubwa na tunatumai kuwa, azimio la Bunge la Iraq kuhusu kuondoka askari wa Marekani litatekelezwa kivitendo."
Kwa upande wake, Faleh al-Fayyad amesema: "Adui alidhani kuwa kwa kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani angeweza kudhuru mapambano na mwamko wa wananchi lakini kile kinachojiri sasa ni kutimuliwa Marekani Iraq na hayo ni mafanikio makubwa."
Ameongeza kuwa: "IRGC ni fahari yetu na ni jukumu letu kutumia uzoefu wake."