Araqchi: Uingereza haitaweza katu kuirubuni Iran kimabavu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, Uingereza inafanya kila njia ili kuirubuni Iran kimabavu mkabala wa kulipa fedha za madeni inayodaiwa na Iran, ambazo inazishikilia kinyume cha sheria kwa zaidi ya miaka 40 sasa.
Sayyid Abbas Araqchi ameyasema hayo katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa twitter kujibu matamshi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na akabainisha kuwa, Uingereza inafanya kila njia ili kuirubuni Iran kimabavu mkabala wa kulipa fedha za madeni inayodaiwa na Iran ambazo inazishikilia kinyume cha sheria kwa zaidi ya miaka 40 sasa, lakini jambo hilo halitatokea katu.
Araqchi amesisitiza kuwa, kwa mtazamo wa Iran makubaliano yaliyofikiwa kabla, yangali yapo pale pale.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, wakati umewadia kwa Uingereza kuchukua hatua sahihi na kutoruhusu Marekani ivuruge mabadilishano hayo ya kibinadamu.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa twitter akidai kuwa, Anousheh Ashouri, mwenye uraiapacha wa Iran na Uingereza na ambaye ameshtakiwa na kuhukumiwa kwa makosa ya ujasusi, alikamatwa kimakosa; na akataka yeye na wafungwa wengine wenye uraia wa Iran na Uingereza wanaoshikiliwa hapa nchini waachiwe huru na kurejea makwao.../