Hafla za maombolezo Iran kwa mnasaba wa Tasu'a ya Imam Hussein AS
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i73636-hafla_za_maombolezo_iran_kwa_mnasaba_wa_tasu'a_ya_imam_hussein_as
Katika usiku wa kuamkia Tasu'a ya Imam Hussein AS, taifa lote la Iran limeghiriki katika maombolezo kwa mnasaba wa siku hii.
(last modified 2026-08-08T07:03:00+00:00 )
Aug 18, 2021 00:02 UTC
  • Hafla za maombolezo Iran kwa mnasaba wa  Tasu'a ya Imam Hussein AS

Katika usiku wa kuamkia Tasu'a ya Imam Hussein AS, taifa lote la Iran limeghiriki katika maombolezo kwa mnasaba wa siku hii.

Leo Jumatano ni tarehe 9 Muharram mwaka 1443 Hijria Qamaria sawa na 18 Agosti 2021 na siku hii ni maarufu kama Tasu'a ya Imam Hussein AS, Imamu wa Tatu wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia ambaye aliuawa shahidi akiwa na wafuasi wake watiifu akiwemo ndugu yake,  Abul Fadhl Abbas AS.

Kwa mnasaba wa kumbukumbu ya yaliyojiri siku ya Tasu'a, kote katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumeshuhudiwa mijumuiko ya maombolezo.

Katika siku kama hii mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas AS akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo, kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Kwa msingi huo siku hii hukumbukwa kama siku ya ushujaa na ujasiri wa Abul Fadhl Abbas AS.

Waombolezaji katika mkesha wa Tasu'a wakiwa katika kikao cha maombolezo huku kanuni za kiafya zikizingatiwa katika kipindi hiki cha janga la COVID-19

Watu 72 waliokuwa katika kambi ya Imam Hussein AS huko Karbala wote waliuawa shahidi  tarehe 10 Muharram yaani Siku ya Ashura, wakiwa pamoja na kiongozi wao katika mapambano ya haki dhidi ya dhulma na uonevu na hivyo wakaweza kuunusuru Uislamu.

Mwaka huu kutokana na janga la COVID-19 vikao vya maombolezo havikufanyika ndani ya misikiti au ndani ya kumbi bali zimefanyika katika maeneo ya wazi ambapo waombolezaji wamezingatia kanuni za kiafya katika kipindi hiki.

Kwa mnasaba wa siku hii ya Tasu'a ya Imam Hussein AS, Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linatuma salamau za rambi rambi kwa Waislamu kote duniani hasa Mashia na wapenda uhuru wengine duniani kote.