Jibu la Iran kwa ripoti mpya ya IAEA
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa, hatua za Iran za kupunguza uwajibikaji wake katika masuala ya nyuklia zinachukuliwa katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Aidha amesema iwapo Marekani na madola mengine yaliyoafiki mapatano ya JCPOA yatatekeleza ahadi zao, basi Iran nayo itarejea katika mkondo wa kutekeleza ahadi zake.
Katika taarifa, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria ripoti ya hivi karibuni ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu shuguli za nyuklia za Iran na kusema hatua zote za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinaenda sambamba na mkataba wa NPT na chini ya usimamizi wa IAEA.
Aidha amesema, hatua za Iran za kupunguza utekelezaji ahadi zake za nyuklia zinahusiana na mapatano ya JCPOA na imechukua hatua hizo kwa mujibu wa mapatano hayo kutokana na hatua ya Marekani ya kukiuka pakubwa mapatano hayo ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Aidha amesema hatua hizo za Iran pia zimechukuliwa kwa sababu pande zingine katika mapatano ya JCPOA hasa nchi tatu za Ulaya nazo pia zimekiuka ahadi zao katika mapatano hayo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, maadamu Marekani na pande zingine katika mapatano ya JCPOA hazitekelezi kikamilifu mapatano hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatekeleza mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani kwa mujibu wa mahitajio yake na maamuzi ya mfumo wa utawala na kwa kuzingatia kanuni za IAEA.
Khatibzadeh pia amesisitiza kwa mara nyingine tena kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni wa malengo ya amani na hauna muelekeo wa kijeshi. Aidha amesema iwapo pande zingine katika mapatano ya JCPOA zitatekeleza ahadi zao kikamilifu na kusitisha vikwazo vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya watu wa Iran, basi Iran nayo itatekeleza kikamilifu ahadi zake katika mapatano hayo.
Siku ya Jumanne, IAEA katika ripoti ilidai kuwa Iran imeongeza kasi ya urutubishaji madini ya urani.