Majeshi ya Majini ya Iran na Pakistan kushirikiana Bahari ya Hindi
Admeli Shahram Irani Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na Makuu wa Jeshi la Majini la Pakistan Admeli Mohammad Amjad Khan Niazi na kusema uhusiano wa majeshi ya majini ya nchi hizi mbili ni wa kistratijia na umekuwa mzuri kwa miaka mingi.
Katika kikao hicho kilichofanyika Jumamosi mjini Tehran, Admeli Shahram Irani amesema nchi hizi mbili jirani zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika masuala ya ubaharia na kuongeza kuwa: "Pakistan inatazamiwa kuendeleza uhusiano huo mzuri wa kihistoria na kuimarisha uhusiano wake na nchi jirani za Kiislamu ambazo zina nukta za pamoja za kiutamaduni na kihistoria.
Akiashiria historia ndefu ya uhusiano wa majeshi ya majini ya Iran na Pakistan, ameongeza kuwa, "Uhusiano wa majeshi ya majini ya Iran umekuwa mzuri na majeshi haya yameweza kufanya mazoezi ya pamoja baharini."
Aidha Admeli Irani amesema majeshi mawili ya majini ya Iran na Pakistan yanapaswa kufanya kazi pamoja kwa ajili ya usalama hasa katika Bahari ya Hindi.
Hali kadhalika ameongeza kuwa, stratijia muhimu zaidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuimarisha diplomasia ya ulinzi na kuongeza kuwa: "Pakistan kama nchi ya kwanza ya Kiislamu ambayo imeweza kupata nguvu za nyuklia ina nafasi maalumu miongoni mwa nchi za Kiislamu."