Iran yapanua wigo wa ulinzi nje ya mipaka yake
Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kupitia taarifa kwamba inaimarisha ilinzi wa nchi nje ya mipaka yake kwa lengo la kuzuia hujuma yoyote inayoweza kufanywa na maadui, kusudio likiwa ni utawala haramu wa Israel na nchi za Magharibi.
Wizara hiyo imesema kupitia taarifa iliyotangaza Siku ya Sekta ya Ulinzi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina jukumu zito la kuimarisha ulinzi wake nje ya mipaka ya nchi kwa madhumuni ya kuboresha uwezo wake wa kukabiliana na maadui.
Taarifa hiyo imesema Iran kamwe haitaacha kuimarisha uwazo wake wa kijeshi yakiwemo makombora ambayo yametengenezwa kwa ajili tu ya kulinda usalama wa nchi.
Jeshi la Iran pia limesema kwamba sekta ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebadilika na kuwa ngome madhubuti ya kutoa jibu kali dhidi ya maadui.
Tarehe 22 Agosti imetengwa kwa ajili ya kutoa fursa ya kuenziwa mashujaa waliotegemea uwazo wa ndani ya nchi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa anga, nchi kavu na majini wa Iran, jambo ambalo limeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa mfano mzuri wa kuigwa na mataifa mengine yaliyo huru na yanayojitawala.
Sekta ya ulinzi ni moja ya sehemu muhimu ambazo maadui wa Iran wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kuidhoofisha na kuzuia ustawi wake kupitia vikwazo mbali mbali tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.