Viwanda ya ulinzi ni nguzo ya uwezo wa Majeshi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i73800-viwanda_ya_ulinzi_ni_nguzo_ya_uwezo_wa_majeshi_ya_iran
Tarehe 31 Mordad kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia sawa na Agosti 22 ni Siku ya Viwanda vya Ulinzi Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 22, 2021 05:07 UTC
  • Viwanda ya ulinzi ni nguzo ya uwezo wa  Majeshi ya Iran

Tarehe 31 Mordad kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia sawa na Agosti 22 ni Siku ya Viwanda vya Ulinzi Iran.

Katika ujumbe kwa mnasaba wa siku hii, Meja Jenerali Mohammad Baqeri Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: “Sera ya kistratijia ya Majeshi ya Iran isiyoweza kusitishwa ni kuimarisha uwezo wa kujihami na kumzuia adui na pia uwezo wa kuhujumu ngome za vitisho dhidi ya taifa hili la Kiislamu. Stratijia hii inatekelezwa bila kuzingatia vita vya vyombo vya habari na oparesheni za kisaikolojia za vyombo vya habari vya mabeberu na pia matarajio yasiyoweza kufikiwa ya Marekani, utawala wa Kizayuni na watitifaki wao khabithi.”

Udharura na umuhimu wa kuimarisha viwanda vya ulinzi au kijeshii unatokana na kuwa maadui wa taifa la Iran wanatumia uwezo wao wote na kila fursa inayojitokeza kutoa vitisho na kuwashinikiza watu wa Iran.

Ingawa maadui wa taifa la Iran, hasa Marekani, wanajizuia kukabiliana ana kwa ana kijeshi na Iran lakini pamoja na hayo haipasi kughafilika na njama wanazotekeleza. Ni kwa msingi huo ndio Majeshi ya Iran yakawa yanatekeleza sera maalumu ya kuimarisha kwa kiwango cha kistratijia uzalishaji silaha na zana za kivita ndani ya nchi kwa lengo la kuwa na uwezo wa kujihami na kumzuia adui kushambulia.

Sekta ya ulinzi nchini Iran ni kati ya sekta muhimu ambazo tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu maadui wamekuwa wakijaribu kuidhoofisha kupitia vikwazo. Lengo la njama  hizo ni kuzuia Iran kustawi katika sekta hii muhimu.

Njama hizo kwa hakika zilikuwa tishio kubwa kwa usalama wa nchi lakini ustawi wa Iran katika sekta ya ulinzi ni ishara kuwa tishio hilo limebadilishwa kuwa fursa kwa ajili ya ustawi wa nguvu za kujihami na kumzuia adui.

Ndege ya kivita ya Kosar iliyoundwa Iran

Antoine Coppolani mtaalamu wa masuala ya ulinzi katika makala aliyoandika katika jarida la Le Point la Ufaranasa anasema: “Katika harakati ya kistratijia, makombora ya Iran yameweza kuboreka na kupata uwezo mkubwa na hivyo Iran imeimarisha nguvu zake za kumzuia adui kushambulia na kukabiliana na hujuma yoyote ile.”

Sekta muhimu ya ulinzi nchini imeweza kustawi kwa msingi wa teknolojia za kisasa. Ni kwa msingi huo ndio mafanikio ya kisayansi na kitekenolojia katika sekta ya ulinzi ya Iran yamepatikana pamoja na kuwa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya nchi hii vinaongezeka. Ustawi wa sayansi na teknolojia katika sekta ya ulinzi ni nukta yenye umuhimu mkubwa kwani huwa ni kama injini ya kustawi sekta nyinginezo za viwanda.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran katika mkutano na makakamanda wa Jeshi la Anga na Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Nchi Kavu la Iran, alisisitiza kuhusu ulazima wa Iran kujiimarisha katika sekta zote  hasa sekta ya ulinzi. Aliendelea kusema kuwa iwapo nchi itakuwa dhaifu basi adui atapata uthubutu wa kuchukua hatua za uchokozi. Aliongeza kuwa: “Sisi hatutaki kuwa tishio kwa nchi  yoyote bali tunataka kulinda usalama wa nchi na kuzuia vitisho.”

Kwa hivyo uwezo wa kijeshi wa Iran umestawi kwa kuzingatia vitisho vya maadui lakini uwezo huo unatumika kwa ajili tu ya kulinda usalama wa nchi.

Leo, kwa mtazamo wa vigezo vya kimataifa vya kijeshi na ulinzi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatazamwa kama dola lenye nguvu na uwezo mkubwa katika eneo la Asia Magharibi. Hatua ya Iran kujiundia makombora ya kisasa kabisa na zana zingine za kivita kwa kutegemea teknolojia ya juu ya ndani ya nchi pamoja na uzoefu wa nchi hii katika vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu ni nukta ambazo sasa zimeibadilisha nchi hii kuwa dola lenye nguvu za kistratijia katika eneo.

Ndege isiyo na rubani (droni) aina ya Fotros iliyoundwa nchini Iran

Iran sasa inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi tano bora duniani katika uundaji wa ndege zisizo na rubani au droni na ni nchi ya pili duniani kuunda droni zenye uwezo wa kukwepa rada.

Katika uga wa usalama katika eneo pia Iran sasa ina mapatano ya kistratijia ya kiulinzi na kiuslama na madola makubwa kama vile Russia, Pakistan na China.

Nukta hiyo ndiyo iliyosisitizwa na Admeli Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumamosi mjini Tehran wakati alipokutana na Admeli Mohammad Amjad Khan Niazi, Kamanda wa Jeshi la Majini la Pakistan.

Admeli Shahram Irani alibaini kuwa: “Stratijia muhimu zaidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuimarisha diplomasia ya ulinzi.”