Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan mjini Tehran; majadiliano kuhusu uhusiano wa pande mbili na matukio ya kieneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i73842
Jana Jumapili, Toshimitsu Motegi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan alionana na kuzungumza mjini Tehran na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 23, 2021 11:29 UTC
  • Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan mjini Tehran; majadiliano kuhusu uhusiano wa pande mbili na matukio ya kieneo

Jana Jumapili, Toshimitsu Motegi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan alionana na kuzungumza mjini Tehran na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika mazungumzo hayo, Rais Raisi huku akisisitiza udharura wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili katika nyanja zote na hasa za uchumi na biashara, amesema kuimarishwa uhusiano na Japan ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan amempongeza Rais Raisi kwa kuanza kipindi chake kipya cha urais na kusisitiza juu ya kuimarishwa zaidi uhusiano mkongwe wa nchi mbili hizi. Amesema Iran na Japan zimekuwa na uhusiano mkongwe na wa kirafiki na kuongeza kuwa hana shaka kuwa uhusiano huo utaendelea kuimarika.

Ukiukaji wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, vikwazo visivyo vya kisheria vya Marekani na taathira zake hasi dhidi ya watu wa Iran, usalama wa eneo na matukio ya karibuni huko Afghanistan ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika mazungumzo ya waziri wa mambo ya nje wa Japan na viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Pamoja na hayo lakini uhusiano wa nchi mbili ulipewa nafasi kubwa zaidi katika mazungumzo hayo.

Waziri Toshimitsu Motegi (kushoto) akiwa ofisini kwa Rais Raisi

Ni kwa kutilia maanani nukta hiyo ndipo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akasisitiza udharura wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote na hasa za uchumi na biashara na kuongeza kwamba suala la kuimarishwa uhusiano wa Iran na Japan linapewa uzito mkubwa katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sehemu nyingine ya umuhimu wa safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan hapa nchini inahusiana na ukiukaji wa Marekani wa mapatano ya JCPOA.

Katika uwanja huo, Rais Rais ameashiria matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan kuhusu umuhimu wa kutekelezwa mapatano ya JCPOA na kusema, kwa kawaida nchi inayoheshimu na kutekeleza wajibu wake inapaswa kushukuriwa na ile inayovunja na kukiuka wajibu huo inapaswa kulaumiwa na kuwajibishwa kisheria. Amesisitiza kwamba Wamarekani wanapasa kujibu jamii ya kimataifa ni kwa nini wamekataa kutekeleza wajibu na ahadi walizotoa katika mapatano ya JCPOA na hatimaye kuamua kujitoa katika mapatano hayo.

Ukweli wa mambo ni kuwa taathira hasi za hatua hiyo ya upande mmoja ya Marekani zinaonekana wazi katika ngazi za kimataifa. Iwapo Ulaya na nchi kama vile China, Japan, Russia na India hazitasimama imara na kueteta haki zao mkabala na siasa za upande mmoja za Marekani ni wazi kuwa jambo hilo litazipelekea nchi hizo kulipa gharama kubwa katika nyanja zote kimataifa.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo yake na Abe Shinzo, Waziri Mkuu wa zamani wa Japan aliyekuwa ameitemebela Iran tarehe 13 Juni 2019 alisema: Japan ni nchi muhimu barani Asia na kama inataka kuimarisha uhusiano wake na Iran inapasa kuwa na nia thabiti katika uwanja huo kama zilivyofanya baadhi ya nchi muhimu.

Uzoefu unaonyesha kwamba kushirikiana na Marekani hakuna manufaa yoyote ya kiusalama kieneo na kimataifa.

Katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran pia alisema kuwa njia pekee ya kujikwamua katika mkwamo uliosababishwa na Marekani ni kudhaminiwa yaki ya taifa la Iran.

Toshimitsu Motegi (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na Mohammad Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran

Hata kama Japan haifichi wasiwasi wake kuhusu hali ya hivi sasa lakini ni wazi kuwa haijachukua hatua yoyote ya maana katika kupinga vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Pamoja na hayo Rais wa Iran amepongeza misaada ya kiutu ya Japan kwa watu wa Iran katika kukabiliana janga la corona na kusisitiza udharura wa kuachiliwa pesa za kigeni za Iran zinazozuiliwa katika benki za Japan. Amesema hakuna sababu yoyote inayohalalisha kuendelea kuzuiliwa fedha hizo.

Ni wazi kuwa jamii ya kimataifa ina jukumu zito la kulinda mapatano ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwa msingi huo inatazamiwa kuwa Japan ambayo ni nchi muhimu na yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi katika ngazi za kimataifa, itatekeleza majukumu yake katika uwanja huo kwa umakini na uwajibikaji zaidi.