Iran yahimiza kuundwa serikali jumuishi Afghanistan, yasema hakuna suluhisho la jeshi
-
Saeed Khatibzadeh
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito kwa vikundi vya Afghanistan kutumia tukio la kuondoka wanajeshi wa Merekani nchini humo kama fursa ya kurejesha amani katika nchi yao, akisema historia ya Afghanistan inaonesha kuwa hakuna suluhisho la kijeshi kwa mizozo ya nchi hiyo.
Saeed Khatibzadeh amesema: Tehran inazitaka pande zote kudumisha utulivu na inatumai kuwa makundi yote yatatumia vyema fursa ya kuondoka vikosi vya mataifa ajinabi nchini Afghanistan kwa ajili ya kuanzisha serikali itaakayoshirikisha makundi yote na kudumisha uhusiano mzuri na majirani wa Afghanistan.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran ameongeza kuwa, yanayojiri sasa nchini Afghanistan yanathibitisha kuwa, mahala popote inapoweka mguu, Marekani hufikiria na kujali tu maslahi yake. Amesema yanayoshuhudiwa Afghanistan ni somo kubwa kwa wale wanaofungamanisha usalama wao na ule wa Marekani. Ameongeza kuwa uwepo wa Marekani nchini Afghanistan haukuwa na faida yoyote ghairi ya kusababisha hasara kubwa, mauaji na umaskini na hatimaye wanajeshi wa nchi hiyo wameondoka Afghanistan kwa njia ya kutisha na kustaajabisha.
Vilevile ameitaka Marekani iheshimu sheria na kanuni za kimataifa.
Wapiganaji wa kundi la Taliban, Jumapili Agosti 15 waliingia mji mkuu wa Afghanistan, Kabul sambamba na kuanguka kwa serikali kufuatia hatua ya Rais Muhammad Ashraf Ghani kuitoroka nchi. Kuporomoka kwa serikali ya Afghanistan kunafuatia makubaliano ya amani yaliyofikiwa baina ya Marekani na Taliban mjini Doha huko Qatar Februari mwaka jana wa 2020.