Iran yazalisha dozi milioni 8 za chanjo ya Coviran Barekat
Kituo cha Habari cha Kitengo cha Utekelezaji wa Maagizo ya Imam Khomeini (M.A) kimetangaza kuwa, dozi milioni 8 za chanjo ya corona ya Coviran Barekat zimezalishwa hapa nchini.
Kituo hicho jana kiliripoti kuwa, hadi kufikia jana jumla ya dozi milioni nane za chanjo ya corona ya Coviran Barekat zimezalishwa hapa nchini. Kimeongeza kuwa, idadi ya chanjo zilizokabidhiwa kwa Wizara ya Afya na Tiba ya Iran hadi kufikia jana Jumatatu ni karibu milioni nne na laki mbili; na kwamba chanjo zilizosalia zinaendelea kupitia mchakato wa kukaguliwa na kutazamwa ubora wake.
Wizara ya Afya na Tiba ya Iran imetangaza kuwa hadi sasa watu milioni 2 elfu 37 na 98 wamepokea dozi ya kwanza ya chanjo ya Coviran Barekat; na 549,838 tayari wamepata dozi ya pili ya chanjo hiyo.
Chanjo hiyo ya UVIKO-19 iliyotengenezwa na watafiti wa Kiirani ilianza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu siku ya Jumanne 29 Disemba mwaka jana ambapo watu waliojitolea walidungwa chanjo hiyo.