Rais wa Iran aomboleza kifo cha Ayatullah Saeed Al Hakim
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74286-rais_wa_iran_aomboleza_kifo_cha_ayatullah_saeed_al_hakim
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kufuatia kuaga dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Mohammad Saeed Tabatabai Hakim wa Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2021 22:04 UTC
  • Rais Sayyid Ebrahim Raisi
    Rais Sayyid Ebrahim Raisi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kufuatia kuaga dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Mohammad Saeed Tabatabai Hakim wa Iraq.

Katika ujumbe wake, Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemuomboleza mwanazuoni na faqihi wa ngazi za juu Ayatullahil Udhma Sayyid Saeed Hakim na kusema: "Marjaa huyu wa kidini alikuwa moja kati ya nguzo za kifiqhi na marjaiya nchini Iraq alikonawiri na alitumia umri wake katika njia ya kueneza Uislamu na fikra za Ahul Bayt (AS)."

Aidha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mapambano ya mwanazuoni huyo wa kidini katika kutetea haki za taifa la Iraq yalipelekea afungwe miaka mingi wakati  wa utawala wa Kibaath wa Saddam Hussein na hivyo katika historia ya mapamabano ya watu wa Iraq anatazamwa kama kielelezo imara cha namna ambavyo Maulamaa wa Kiislamu daima wako pamoja na wananchi.

Marhum Ayatullahil Udhma Sayyid Mohammad Saeed Tabatabai Hakim 

Rais Ebrahim Raisi amesema Ayatullah Sayyid Mohammad Saeed Tabatabai Hakim pamoja na watu wengine wa ukoo mkubwa wa Hakim alikuwa na nafasi kubwa katika kuwatetea  wananchi wa Iraq na kuwawezesha kupata uhuru na kujitegemea sambamba na kuhakikisha wananchi wenyewe wanajiamulia hatima yao wakiwa na umoja katika Iraq mpya.

Ayatullah Sayyid Mohammad Saeed Tabatabai Hakim Marjaa Taqlid maarufu katika mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq aliaga dunia Ijumaa iliyopita kutokana na mshtuko wa moyo.