Raisi: Usalama na amani ya nchi jirani ni usalama wa Iran
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo na katika mazungumzo yake ya kwanza mubashara na wananchi kupitia televisheni ya taifa amesema Jamhuri ya Kiislamu inatambua amani na usalama wa nchi jirani kuwa ni amani na usalama wake na kuongeza kuwa, hadi sasa amefanya mazungumzo va vikao zaidi ya 50 na viongozi wa nchi mbalimbali na kwamba vikao na mazungumzo hayo yamejikita katika suala la kuwepo ushirikiano.
Katika mazungumzo hayo ya jana usiku Ayatullah Sayyid Ebrahim Raisi aliashiria hali ya sasa nchini Afghanistan na kusema: Ufumbuzi wa hali ya Afghanistan ni kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi na kutangulizwa mbele matakwa yao.
Amesema Iran daima inataka kuwepo amani na utulivu na kutawala matakwa ya wananchi huko Afghanistan na kuongeza kuwa, serikali itakayotokana na rai na matakwa ya wananchi katika nchi hiyo inaweza kuwa na uhusiano mwema na Iran. Amesisitiza kuwa, kadhia ya Afghanistan imeonesha kuwa, kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini humo hakukurejesha amani bali kumeififiza na kuivuruga zaidi.
Kuhusu mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na nchi wanachama katika makubaliano ya JCPOA, Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa, mazungumzo ni wenzo wa kidiplomasia, na Iran haipingi suala hilo japokuwa Wamagharibi na Marekani wanataka kutumia mazungumzo sambamba na mashinikizo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kuishinikiza Iran hakujawahi kuzaa matunda na Wamagharibi wamejaribu wenzo huo mara nyingi. Amesisitiza kuwa mazungumzo yanayoandamana na mashinikizo hayakubaliki.