Iran: Tuko pamoja na wananchi wa Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74356-iran_tuko_pamoja_na_wananchi_wa_afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Tehran itaendelea kuwa pamoja na wananchi wa Afghanistan katika juhudi za kuleta amani na utulivu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 06, 2021 06:39 UTC
  • Iran: Tuko pamoja na wananchi wa Afghanistan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Tehran itaendelea kuwa pamoja na wananchi wa Afghanistan katika juhudi za kuleta amani na utulivu nchini humo.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na huku akijibu swali la mwandishi wa shirika la habari la Iran Press amesema kuwa, wawakilishi maalumu wa masuala ya Afghanistan katika wizara za mambo ya nje za nchi jiran wamewasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdolahian na kujadiliana kwa kina masuala ya Afghanistan.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Tehran inawasaidia wananchi wa Afghanistan kutatua migogoro yao na kuleta amani kwa mujibu wa sheria na ombi la Afghanistan.

Mapigano katika eneo la Panjshir, Afghanistan

 

Amma kuhusiana na eneo la Panjshir, Khatibzadeh amesema, taarifa zinazotolewa kuhusu Taliban kushambulia eneo hilo zinataia wasiwasi sana. Mashambulio yaliyofanywa kwenye eneo hilo na kuuawa shahidi viongozi wa Afghanistan, yanasikitisha sana. Suala la uingiliaji wa kigeni linachunguzwa. Kila mtu anapaswa kuielewa vizuri historia ya Afghanistan ambayo imethibitisha kwamba mara zote uingiliaji wa kigeni umefeli na kushindwa nchini humo.

Amesema, wananchi wa Afghanistan ni watu wenye ghera na wanaopenda kuwa huru. Iran inalaani uingiliaji wowote wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Suala la Panjshir linaweza kutatuliwa kwa njia za kisiasa, mazungumzo na upatanishi. Mtu yeyote hapaswi kudharau uhakika huo na kutumia njia ambazo hazina matokeo mengine zaidi ya kupalilia chuki na uhasama. Taliban wanapaswa kuheshimu ahadi zao. Tumepokea habari kuwa Taliban wamelizingira eneo la Panjshir. Tutambue kuwa kuwakatia watu umeme na kuwatumbukiza kwenye njaa na umaskini na tabu nyinginezo, ni kinyume na sheria za kimataifa.