Abdollahian: Marekani ndiye mhalifu mkuu katika ukiukaji wa JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74372-abdollahian_marekani_ndiye_mhalifu_mkuu_katika_ukiukaji_wa_jcpoa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Marekani imetoa pigo kuu kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA; na si mtuhumiwa bali ndiye mhalifu mkuu katika ukiukaji wa makubaliano hayo.
(last modified 2026-08-08T07:03:00+00:00 )
Sep 06, 2021 22:57 UTC
  • Abdollahian: Marekani ndiye mhalifu mkuu katika ukiukaji wa JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Marekani imetoa pigo kuu kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA; na si mtuhumiwa bali ndiye mhalifu mkuu katika ukiukaji wa makubaliano hayo.

Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mkutano na mabalozi na wawakilishi wa nchi za kigeni walioko hapa nchini ambapo sambamba na kusisitiza kuwa Tehran inakaribisha mazungumzo yoyote yatakayolihakikishia taifa adhimu la Iran kupata haki na maslahi yake, ameongezea kwa kusema: "Sisi tunataka mazungumzo ya busara, makini na yanayodhamini haki za taifa la Iran na tunachukua hatua kivitendo juu ya suala hili."

Abdollahian amesema: "Sisi hatuyaoni kuwa na faida kwa taifa la Iran mazungumzo yasiyo na tija na ya upotezaji muda."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria pia matukio yanayojiri nchini Afghanistan, ambapo mbali na kudokeza kwamba Tehran inawasiliana na pande zote nchini humo, ametilia mkazo pia kuundwa serikali pana itakayoshirikisha makabila yote ya Afghanistan.

Hossein Amir-Abdollahian

Vilevile Amir Abdollahian amezungumzia kuwepo kwa suitafahamu katika uhusiano wa pande mbili kati ya Iran na nchi chache, suitafahamu ambazo zimekwamisha harakati chanya na kupatikana uhusiano mzuri na unaotakikana wa kidiplomasia na akasisitiza juu ya kupewa umuhimu mantiki ya mazungumzo kwa kusema: "Sisi tunayachukulia mazungumzo na nchi za kanda kuwa ni msingi mkuu na tunaamini mazungumzo ya ndani ya eneo ndio njia mwafaka ya kuondokana na hali inayotawala hivi sasa katika kanda hii."

Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia suala la uhusiano wa Iran na Ulaya ambapo mbali na kusisitiza kuhusu fursa ilizonazo Ulaya na Magharibi katika sera za nje zenye mlingano za serikali mpya ya Iran amesema: Ulaya si Troika pekee.

Aidha amesema, nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinazounda Troika hiyo ya Ulaya inapasa ziondokane na hali ya kutochukua hatua za kivitendo katika kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.../