Diplomasia ya Tehran; juhudi za kusaidia mchakato wa mazungumzo shirikishi nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74430-diplomasia_ya_tehran_juhudi_za_kusaidia_mchakato_wa_mazungumzo_shirikishi_nchini_afghanistan
Siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kusaidia mchakato wa mazungumzo ya makundi na vyama vyote huko Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 08, 2021 11:03 UTC
  • Diplomasia ya Tehran; juhudi za kusaidia mchakato wa mazungumzo shirikishi nchini Afghanistan

Siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kusaidia mchakato wa mazungumzo ya makundi na vyama vyote huko Afghanistan.

Kuhusiana na suala hilo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi jirani na Afghanistan leo wamefanya kikao kwa njia ya intaneti chini ya usimamizi wa Iran. Nukta muhimu katika kikao hicho ni kuona nchi jirani na Afghanistan zinafanikiwa kupata njia na ubunifu ili kuhitimisha hali ya mivutano na kurejesha amani ya kudumu nchini Afghanistan. Ukweli ni kuwa, Afghanistan ni mhanga wa sera za uingiliaji kati na uvamizi wa miaka 20 wa Marekani ambao matokeo yake ni vita na ukosefu wa amani unaoshuhudiwa sasa katika nchi hiyo.  

Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema hivi karibuni hapa Tehran katika mazungumzo yake na Shah Mahmood Qureshi Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan kuwa: Kuondoka Marekani huko Afghanistan ni tukio muhimu kwa ajili ya kurejeshwa ushirikiano baina ya kaumu na makundi ya Kiafghani na kuimarisha amani na utulivu nchini humo. Kuhusiana na kikao cha Tehran tunapaswa kuashiria nukta mbili muhimu.

Nukta ya kwanza ni udharura wa kujiepusha na machafuko na mapigano baina ya wanandugu, na pili ni ulazima wa kutilia maanani masaibu na matatizo ya wananchi wa Afghanistan. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan katika mazungumzo na Rais Ebrahim Raisi 

Alireza Salimi mjumbe wa Bodi ya Uongozi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi jirani na Afghanistan na kueleza kuwa: "Sera ya Iran kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni kuyaunga mkono mataifa mbalimbali na kwamba Iran ya Kiislamu sasa ina wasiwasi kuhusu hali ya taifa la Afghanistan."   

Alireza Salimi amesisitiza pia umuhimu wa kulindwa haki za taifa lote la Afghanistan na si za kundi makhsusi. Amesema anaamini kuwa, kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi jirani na Afghanistan kinaweza kuandaa njia ya kuondoa mivutano iliyopo na kusaidia jitihada za kupatikana haki za wananchi wote wa Afghanistan.  

Kwa hivyo inatarajiwa kuwa kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi jirani na Afghanistan kinatoa ujumbe wa wazi na wenye nguvu ili kuwezesha kuasisiwa serikali shirikishi nchini Aghanistan. Tehran iko tayari kusaidia mchakato wa kurejesha amani na utulivu huko Afghanistan katika fremu ya diplomasia ya kikanda na kimataifa, na kuhusu hilo inafanya juhudi za kuhitimishwa masaibu yanayowapata wananchi wa Afghanistan na kuundwa serikali shirikishi yenye kuakisi muundo wa kikabila na kijamii nchini humo.  

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh pia amesisitiza kuwa, kadhia ya Panjshir inaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya kisiasa na kwamba kuzingirwa eneo hilo hakukubaliliki katika mtazamo wa sheria za kimataifa na kibinadamu. Khatibzadeh amelaani uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya Afghanistan na kueleza kuwa: "Wale wanaofanya makosa ya kistratejia wanapaswa kuelewa kuwa, jiografia ya Afghanistan ni jiiografia ya wananchi ambao wako tayari kupigana vita kuvifukuzilia mbali vikosi vamizi."  

Wakati huo huo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hatua ya kuwasababishia njaa wakazi wa Panjshir, kuwazingira na kuwakatia huduma ya maji na umeme ni mambo yenye kutia wasiwasi na amelitaka kundi la Taliban kuheshimu ahadi  na matamko yake yote ya huko nyuma.

Ni wazi kuwa amani na usalama haviwezi kupatikana katika ardhi ya Afghanistan isipokuwa kwa kutilia maanani matakwa ya wananchi na kuundwa serikali itakayoshirikisha vyama na makundi yote ya nchi hiyo. Na katika hali ya sasa hakuna njia nyingine ghairi ya kufanyika mazungumzo ili kufikiwa mapatano kati ya makundi na kaumu zote nchini humo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, Waafghani wenyewe ndio wanaopasa kuchukua maamuzi kuhusu mustakbali wa nchi yao. 

Taliban baada ya kuvamia Panjshir