Amir-Abdollahian: Iran inataka kuundwe serikari jumuishi nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74478-amir_abdollahian_iran_inataka_kuundwe_serikari_jumuishi_nchini_afghanistan
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu bado inafuatilia suala la kuundwa serikali jumuishi na inayoshirikisha makundi na kaumu zote huko nchini Afghanistan.
(last modified 2026-08-11T03:40:48+00:00 )
Sep 09, 2021 22:17 UTC
  • Amir-Abdollahian: Iran inataka kuundwe serikari jumuishi nchini Afghanistan

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu bado inafuatilia suala la kuundwa serikali jumuishi na inayoshirikisha makundi na kaumu zote huko nchini Afghanistan.

Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo jana katika kikao cha nchi sita jirani na Afghanistan na kuongeza kuwa, Iran bado inafuatilia suala la kuundwa serikali jumuishi inayoshirikisha kaumu zote, na ina matumaini kwamba, kundi la Taliban litatekeleza ahadi yake. 

Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, tajiriba imethibitisha kuwa, kuunda serikali isiyoshirikisha makundi yote ya jamii hakuwezi kusaidia juhudi za kurejesha amani na usalama na kuboresha maisha ya Waafghani. 

Amesema inatarajiwa kuwa mawazirii wa mambo ya nje wa nchi jirani na Afghanistan watapaza sauti zao kusisitiza umuhimu wa kuundwa serikali jumuishi itakayoshirikisha makundi na kaumu zote za nchi hiyo. 

Viongozi wa Taliban watakiwa kuunda serikali jumuishi

Vilevile amesisitiza kuwa Marekani ndiyo sababu kuu ya matatizo ya kipindi chote cha miaka 20 ya uvamizii wa nchi hiyo huko Afghanistan na kwamba Washington inapaswa kuwajibishwa mbele ya walimwengu kwa sababu katika kipindi cha kuwepo wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan ulanguzi na biashara ya dawa za kulevya imeongezeka mara kadhaa. 

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema, Marekani inadai kuwa imetumia dola trilioni 6 nchini Afghanistan lakini matokeo yake ni umaskini, hali mbaya na ukosefu wa amani.