Iran na IAEA zasisitiza kuimarisha ushirikiano wa kiufundi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74574-iran_na_iaea_zasisitiza_kuimarisha_ushirikiano_wa_kiufundi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) leo zimetoa taarifa ya pamoja zikitilia mkazo suala la kuimarisha ushirikiano wa kiufundi baina ya pande hizo mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2021 06:09 UTC
  • Iran na IAEA zasisitiza kuimarisha ushirikiano wa kiufundi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) leo zimetoa taarifa ya pamoja zikitilia mkazo suala la kuimarisha ushirikiano wa kiufundi baina ya pande hizo mbili.

Taarifa hiyo ambayo imetolewa leo baada ya mazungumzo ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Rafael Grossi na Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran, Mohammad Eslami imesisitiza kuimarishwa ushirikiano wa kiufundi baina ya Iran na wakala huo katika nyanja mbalimbali za masuala ya nishati ya nyuklia. Taarifa hiyo imesema: Pande mbili zinasisitiza na kukumbusha udharura wa kuwepo moyo wa ushirikiano na kuaminiana na vilevile umuhimu wa kushughulikiwa masuala yao katika anga nzuri na kwa kutilia maanani masuala ya kiufundi. 

Taarifa hiyo ya pamoja pia imesema kuwa, wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki wataruhusiwa kutoa huduma za kiufundi katika maeneo yaliyoainishwa na pande mbili.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki aliwasili mjini Tehran jana usiku. 

Awali msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran alisema kuwa, baadhi ya nchi zinafanya njama za kuyasiasisha masuala ya kiufundi baina ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kuongeza kuwa, inatarajiwa safari ya Grossi mjinii Tehran itakuwa na matunda ya kuridhisha.