Khatibzadeh: Iran haitastahamili vitisho vya aina yoyote dhidi ya usalama wake
-
Saeed Khatibzadeh
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, lengo la mashambulizi yaliyofanywa na Iran hivi karibuni dhidi ya makundi ya kigaidi huko Kurdistan nchini Iraq ni kujibu chokochoko za magaidi hao.
Mapema leo Saeed Khatibzadeh amewaambia waandishi habari mjini Tehran kwamba, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) limeshambulia kambi za makundi ya kigaidi katika eneo la Kurdistan nchini Iraq likijibu mauaji yaliyofanywa na wananchama wa makundi hayo dhidi ya wanajeshi kadhaa huko Iraq na katika mipaka ya Iran ya nchi hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameongeza kuwa, Tehran inayakaribisha makundi ya kigaidi yaliyojuta na ambayo hayataki tena kutumiwa vibaya na madola ya kigeni. Amesisitiza kuwa, Iran inataka kuimarisha amani na usalama.
Kuhusu mazungumzo ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hapa mjini Tehran, Khatibzadeh amesema kuwa, taarifa ya pamoja iliyotolewa jana imeweka wazi kila kitu. Amesema kuwa, Tehran inafuatilia kwa karibu kikao kijacho cha Baraza la Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Baada ya ziara yake mjini Tehran, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ameyataja mazungumzo yake na viongozi wa Iran kuwa chanya na kueleza kuwa, pande mbili zinapiga hatua nzuri katika kuzipatia ufumbuzi hitilafu za kimitazamo.