Rais Ebrahim Rais afanya mazungumzo na viongozi wa Pakistan, Uzbekistan na Belarus
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74734-rais_ebrahim_rais_afanya_mazungumzo_na_viongozi_wa_pakistan_uzbekistan_na_belarus
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili katika mji mkuu wa Tajikistan, Dushanbe, ambako anashiriki mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai unaofanyika nchini humo leo na kesho.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Sep 16, 2021 10:47 UTC
  • Waziri Mkuu wa Pakistan akizungumza na Rais Ebrahim Raisi
    Waziri Mkuu wa Pakistan akizungumza na Rais Ebrahim Raisi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili katika mji mkuu wa Tajikistan, Dushanbe, ambako anashiriki mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai unaofanyika nchini humo leo na kesho.

Baada ya kuwasili Dushanbe, Rais Ebrahim Raisi amelakiwa na Waziri Mkuu wa Tajikistan, Kokhir Rasulzoda.

Hii ni safari ya kwanza ya Rais Sayyid Ebrahim Raisi nje ya nchi tangu alipochukua madaraka ya nchi baada ya kushinda uchaguzi wa Rais wa Juni mwaka huu. Rais Raisi ameelekea Tajikistan akiitikia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Emomali Rahmon na mbali na kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, vilevile anakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi mbalimbali wanaohudhuria mkutano huo. 

Habari zinasema Rais wa Jamhuri ya Kiislamu tayari amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan na Rais wa Uzbekistan, Shavkat Mirziyoyev.

Rais Sayyid Raisi akiwa pamoja na Rais wa Uzbekistan, Shavkat Mirziyoyev

Ajenda kuu ya mazungumzo ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu na viongozi hao imetajwa kuwa ni uhusiano wa pande mbili, uchumi, masuala ya kieneo na ushirikiano wa kimataifa.

Rais Ebrahim Raisi alitarajiwa pia kufanya mazungumzo ya pande mbili na mwenyeji wake, Rais Emomali Rahmon.

Rais Ebrahim Raisi anafutana na ujumbe wa ngazi ya juu wa maafisa wa kisiasa na kiuchumi wa Iran katika safari hiyo huko Tajikistan.

Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai iliasisiwa mwaka 2001 kwa lengo la kukabiliana na ugaidi na vitendo vya uchupaji mipaka na kuimarisha ushirikiana wa kiuchumi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni wanachama watazamaji katika jumuiya hiyo.