Iran: Tehran itaimarisha udiplomasia athirifu katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74780-iran_tehran_itaimarisha_udiplomasia_athirifu_katika_jumuiya_ya_ushirikiano_ya_shanghai
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imezishukuru nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) kwa kuikubali Jamhuri ya Kiislamu kama mwanachama kamili katika jumuiya hiyo na kusema kuwa: Tehran itatumia demokrasia athirifu kwa ajili ya kuimarisha mahusiano na nchi wanachama.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Sep 17, 2021 22:38 UTC
  • Iran: Tehran itaimarisha udiplomasia athirifu katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imezishukuru nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) kwa kuikubali Jamhuri ya Kiislamu kama mwanachama kamili katika jumuiya hiyo na kusema kuwa: Tehran itatumia demokrasia athirifu kwa ajili ya kuimarisha mahusiano na nchi wanachama.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na wizara hiyo ilisema kuwa, baada ya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa kutaka Iran kuwa mwanachama kamili katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai hatimaye na sambamba na kushiriki Rais Sayyid Ebrahim Raisi katika mkutano wa 21 wa viongozi wa nchi wanachama katika mji wa Dushanbe huko Tajikistan, nchi zote 8 wanachama wa SCO zimeikubali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sauti moja kuwa mwanachama wa kudumu katika jumuiya hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imefurahishwa na mafanikio hayo na inaahidi kutumia nyenzo zote za kiufundi kushirikiana na asasi zote za Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) ikiwa ni pamoja na Sekretarieti ya jumuiya hiyo ili kukamilisha mchakato wa kuwa mwanachama kamili katika kipindi kifupi. 

Rais Sayyid Ebrahim Raisi katika mkutano wa Dushanbe

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesisitiza kuwa, kukubaliwa uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni hatua muhimu ambayo itakuwa na nafasi chanya katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi wanachama katika mahusiano ya pande mbili, kikanda na kimataifa. 

Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni China, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Russia, Tajikistan, Uzbekistan, India na Pakistan.

Iran ilikuwa mwanachama mtazamaji tu kabla ya kukubaliwa kuwa mwanachama wa kudumu katika jumuiya hiyo katika kikao cha jana mjini Dushanbe.