Magaidi 2 wa ISIS wakamatwa magharibi mwa Iran wakielekea Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i7612-magaidi_2_wa_isis_wakamatwa_magharibi_mwa_iran_wakielekea_tehran
Vikosi vya usalama vya Iran vimewakamata magaidi wawili wa kundi la wakufurishaji wa ISIS au Daesh katika mkoa wa Hamadan magharibi mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2016 23:06 UTC
  • Vikosi vya ulinzi wa mpakani Iran
    Vikosi vya ulinzi wa mpakani Iran

Vikosi vya usalama vya Iran vimewakamata magaidi wawili wa kundi la wakufurishaji wa ISIS au Daesh katika mkoa wa Hamadan magharibi mwa nchi.

Kwa mujibu wa mkuu wa usalama mkoani, humo magaidi hao raia wa Iran wenye mfungamano na kundi la ISIS walikamatwa katika oparesheni mbili za kiusalama wakiwa wanajitayarisha kuelekea katika mji mkuu, Tehran. Taarifa zaidi kuhusu oparesheni hiyo hazikutolewa.

Ijumaa iliyopita Waziri wa Usalama wa Iran Mahmoud Alavi alifichua kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesambaratisha zaidi ya makundi 20 ya magaidi ambao walikuwa wamepanga kuripua mabomu na kutekeleza hujuma kadhaa kote nchini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Waziri Alavi aliongeza kuwa idadi kubwa ya silaha zilikamatwa mikononi mwa magaidi hao. Halikadhalika amesema vikosi vya usalama vya Iran vimefanikiwa kugundua maeneo ambamo magaidi walikuwa wakitengengeza mabomu.

Aidha alisema Iran ina usalama wa hali ya juu katika hali ambayo nchi nyingi za Mashariki ya Kati na dunia zinakumbwa na ukosefu wa usalama.

Alibainisha kuwa pamoja na kuwepo njama za magaidi na mashirika ya kijasusi ya nchi adui, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kujidhaminia usalama na amani.

Mwezi Aprili pia Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, wanachama wa kundi la kigaidi la ISIS walijaribu kupenya ili waingie Iran lakini jaribio lao hilo likafeli.