Iran haitakubali chochote isipokuwa JCPOA katika mazungumzo ya Vienna
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i77926-iran_haitakubali_chochote_isipokuwa_jcpoa_katika_mazungumzo_ya_vienna
Kiongozi wa ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna amesema:"Iran haitakubali chochote isipokuwa JCPOA"
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 12, 2021 01:07 UTC
  • Iran haitakubali chochote isipokuwa JCPOA katika mazungumzo ya Vienna

Kiongozi wa ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna amesema:"Iran haitakubali chochote isipokuwa JCPOA"

Ali Baqeri Kani Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye anaongoza timu ya Iran katika mazungumzo na kundi la 4+1 amesema katika mazungumzo na televisheni ya Press TV kuwa maudhui ambazo ziliibua hitilafu katika duru sita za mazungumzo zilizopita mjini Vienna bado hazijatatuliwa na ziko juu ya meza.

Ameongeza kuwa, matini rasmi ambayo imewasilishwa baada ya mazungumzo ya duru sita inaashiria maudhui kadhaa ambazo hazijatatuliwa baina ya pande mbili na kuna haja ya maamuzi kuchukuliwa katika ngazi za juu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa ameongeza kuwa baadhi ya masuala hayo yamejadiliwa katika mazungumzo ya siku chache zilizopita ambapo baadhi ya nukta zimekubaliwa na baadhi zimekataliwa na pande husika.

Kuhusu madai ya wakuu wa Marekani kuwa walisema wazi katika mazungumzo yaliyopita kuwa vikwazo vyote haviwezi kuondolewa amebaini kuwa, katika duru hii ya mazungumzo hatuwezi kutoa tathmini ya mapema kuhusu mwenendo wa Marekani bali tutasubiri tuone mweleko mpya watakaochukua.

Duru ya saba ya  kikao hicho cha mapatano ya  JCPOA ilianza 29 mwezi uliopita wa Novemba katika mji mkuu wa Austria, Vienna.  Mazungumzo hayo ni baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 kuhusu kuondolewea vikwazo, hasa  vya Marekani dhidi ya Iran. Nchi za 4+1 ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya.

Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unashiriki katika  mazungumzo huko Vienna kwa mujibu wa haki yake ya kisheria katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kile inachotaka ni kuondolewa vikwazo vyote kwa njia ambayo itaweza kuthibitishwa kivitendo.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza mara kadhaa kwamba, lengo kuu la Tehran la kushiriki mazungumzo ya Vienna kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA  ni kuhakikisha kuwa taifa hili linaondolewa vikwazo vyote haramu.