Khatibzadeh: Mauaji ya Jenerali Soleimani yalikuwa ni ugaidi wa kiserikali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78520-khatibzadeh_mauaji_ya_jenerali_soleimani_yalikuwa_ni_ugaidi_wa_kiserikali
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kitendo cha Marekani cha kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani kilikuwa ni hujuma ya kigaidi na ugaidi wa kiserikali na ametaka wale wote waliohusika na jinai hiyo ya kinyama wapandishwe kizimbani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 27, 2021 10:00 UTC
  • Khatibzadeh: Mauaji ya Jenerali Soleimani yalikuwa ni ugaidi wa kiserikali

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kitendo cha Marekani cha kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani kilikuwa ni hujuma ya kigaidi na ugaidi wa kiserikali na ametaka wale wote waliohusika na jinai hiyo ya kinyama wapandishwe kizimbani.

Akizungumza Jumatatu katika mkutano wa kila wiki na waandishi habari, Saeed Khatibzadeh ameashiria kukaribia kumbukumbu ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Soleimani na kusema: "Luteni Jenerali Soleimani alikuwa ni shujaa katika vita dhidi ya ugaidi." 

Amesema kuuawa kamanda huyu mashuhuri wa vita dhidi ya ugaidi ni thibitisho tosha la undumakuwili na kukosekana ukweli miongoni mwa baadhi ya wale wanaodai kupambana na ugaidi.

Aiadha amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa waliotenda jinai hiyo wanafikishwa kizimbani.

Khatibzadeh amesema mauaji ya kigaidi ya Kamanda Soleimani si tu ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na sheria za kimataifa bali pia ni kitendo cha kivamizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala nchi, yaani Iraq.

Saeed Khatibzadeh

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, ambaye Januari 3 mwaka 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi la kigaidi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Hujuma hiyo ilitekelezwa kufuatia amri ya rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump.

Khatibzadeh amesema kumeundwa kamati ya pamoja ya Iran na Iraq kwa ajili ya kufuatilia waliotekeleza ugaidi huo ili kuhakikisha kuwa wanapandishwa kizimbani.

Aidha amesema kuna haja ya kukabiliana na propaganda za maadui ili kuhakikisha kuwa, fikra za Shahidi Soleimani zinabakia hai.