Jenerali wa Marekani akiri, Iran ina uwezo mkubwa wa makombora
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78548-jenerali_wa_marekani_akiri_iran_ina_uwezo_mkubwa_wa_makombora
Kamanda wa Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) amekiri kuwa Iran ina uwezo mkubwa wa makombora na kusisitiza kwamba makombora ya Iran yanaweza kupiga eneo lolote wanalotaka kwa umakini na kiwango kikubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 28, 2021 06:20 UTC
  • Jenerali wa Marekani akiri, Iran ina uwezo mkubwa wa makombora

Kamanda wa Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) amekiri kuwa Iran ina uwezo mkubwa wa makombora na kusisitiza kwamba makombora ya Iran yanaweza kupiga eneo lolote wanalotaka kwa umakini na kiwango kikubwa.

Jenerali Kenneth F. McKenzie amesema katika mahojiano yake na The New Yorker  kuhusiana na mashambulizi ya makombora ya Iran yaliyolenga kambi kubwa zaidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ya Ainul Asad kwamba: "Miongo kadhaa iliyopita, makombora ya Iran hayakuwa ya hali ya juu na makini, lakini sasa yanaweza kulenga eneo zima la Magharibi mwa Asia, kwa umakini na kiwango kikubwa."

Jenerali McKenzie amekiri kwamba Iran ni nguvu kubwa ya makombora na kusema: Wakati wa hujuma dhidi ya kambi ya kijeshi ya Ainul al- Assad Wairani walipiga karibu kila mahala walipokusudia kulenga.

Jenerali, Kenneth F. McKenzie

Baada ya mahojiano hayo Jarida la New Yorker liliripoti kwamba, Tehran imepita kiwango ambacho Jenerali McKenzie amekiita cha uwezo wa silaha ambao ni vigumu sana kwa nchi nyingine kuushinda au kuudhibiti.

Katika kujibu mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na wanajeshi wa Marekani dhidi ya Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilivurumisha makombora kadhaa katika kambi ya Marekani ya Ain al-Assad nchini Iraq, likiwa ni shambulio la kwanza katika kambi ya Marekani tangu wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.