Raisi: Hezbullah na muqawama umeimarika zaidi Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78660-raisi_hezbullah_na_muqawama_umeimarika_zaidi_asia_magharibi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa: Hizbullah na harakati ya muqawama zina nguvu kubwa zaidi katika eneo hili la Asia Magharibi.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Dec 31, 2021 04:49 UTC
  • Sayyid Ebrahim Raisi
    Sayyid Ebrahim Raisi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa: Hizbullah na harakati ya muqawama zina nguvu kubwa zaidi katika eneo hili la Asia Magharibi.

Sayyid Ebrahim Raisi ambaye alikuwa akizungumza na familia za mashahidi wa Vita vya Kujitetea Kutakatifu na Walinzi wa Haram Tukufu katika mji wa Qum ameashiria tukio la kufukuzwa Wamarekani huko Syria, Afghanistan na Iraq na kusema: Hii leo Wamarekani wamekuwa dhaifu kuliko hapo awali na vikosi vya Hizbullah na Mujahidina wakiwemo wa Palestina ndivyo vyenye mkono wa juu na nguvu zaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Rais Ebrahim Raisi ameongeza kuwa, mashahidi walidhamini usalama wa eneo hili la Magharibi mwa Asia, na hali nzuri iliyopo hivi sasa imepatikana kutokana na damu ya mashahidi, lakini maadui wameendeleza njama zao na sasa wanawahamisha wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) kutoka Syria na kuwapeleka Afghanistan.

Vilevile ameashiria matukio ya Afghanistan na kusema: "Usalama wa Afghanistan ni usalama wa Jamhuri ya Kiislamu, na ukosefu wa usalama huko ni ukosefu wa usalama nchini Iran."

Raisi amesema: Takriban Waafghani milioni 4 wanaishi Iran, na maisha ya Wairani na Waafghani yamefungamana kiasi kwamba ni vigumu kutofautisha baina yao.

Rais wa Iran ameendelea kusema: Daesh ni pandikizi la Wazayuni, na wanachama wake wanafanya kazi kwa niaba kwa ajili ya kufanya uharibifu katika eneo la Asia Magharibi. Ameongeza kuwa kundi hilo linaripua na kuharibu hata misikiti na kuua Waislamu, kazi ambayo pia inafanywa na Wazayuni maghasibu. 

Vilevile amemuenzi Shahidi Qasem Soleimani aliyekuwa kinara wa mapambano dhidi ya kundi la kigaidi al Daesh na kusema: Kamanda Soleimani hakuwa peke yake, bali aliwakilisha mfumo na skuli ya Abu Abdillah, Hussein bin Ali (as).