Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu: Waislamu waungane kupambana na mabeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78720-jumuiya_ya_kukurubisha_madhehebu_waislamu_waungane_kupambana_na_mabeberu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kuwa, umoja na mshikamano baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni ndiyo stratijia kuu ya kuweza kufelisha njama za maadui wa Uislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 02, 2022 00:56 UTC
  • Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu: Waislamu waungane kupambana na mabeberu

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kuwa, umoja na mshikamano baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni ndiyo stratijia kuu ya kuweza kufelisha njama za maadui wa Uislamu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Hujjatul Islam Walmuslimin Hamid Shahriari alisema hayo jana Jumamosi katika kongamano la Umoja wa Kiislamu lililofanyika mjini Lahore, Pakistan na kuongeza kuwa, Waislamu duniani lazima waungane na kuwa kitu kimoja kama wanataka kweli kufelisha ubeberu wa madola ajinabi ambayo lengo lao hasa ni kupora mali na utajiri wa mataifa ya Waislamu.

Amsema, mfumo mtukufu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unalipa umuhimu mkubwa mno suala la kuungana Waislamu na kuwa kitu kimoja bila ya kuzingatia tofauti ndogondogo zilizopo baina yao kwani Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa, hiyo ndiyo njia pekee ya kuuletea hadhi na heshima kubwa umma wa Kiislamu.

Hujjatul Islam Walmuslimin Hamid Shahriari

 

Maulamaa wa Kishia na Kisuni wanaoshiriki kwenye kongamano hilo nao wote wamehimiza na kutilia mkazo wajibu wa kuungana na kushikamana umma wa Kiislamu na kujiweka mbali na sababu pamoja na magenge yanayofanya njama za kuwagombanisha Waislamu. Maulamaa hao wamesema, ni wajibu wa kila Muislamu kuhakikisha anajiepusha kikamilifu na jambo lolote lile ambalo linaweza kuhatarisha ushirikiano na mshikamano baina ya Waislamu.

Maulamaa hao wa Kishia na Kisunni pia wamesema: Kukutana maulamaa wa madhaehebu zote za Kiislamu hakuna matunda mengine ghairi ya kuzidi kushikamana Waislamu na hatimaye kufelisha na kuzishinda njama zote za maadui wa pamoja wa dini hii takatifu.