Khatibzadeh: Hati ya ushirikiano kati ya Iran na Russia inaongezwa muda wake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78798-khatibzadeh_hati_ya_ushirikiano_kati_ya_iran_na_russia_inaongezwa_muda_wake
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, baadhi ya nyaraka na hati za mapatano kati ya Iran na Russia zinafuatiliwa na kwamba hati ya juu ya kuweka sawa uhusiano wa kistratejia kati ya nchi mbili ingalipo na sasa inaongezwa muda wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 03, 2022 23:17 UTC
  • Khatibzadeh: Hati ya ushirikiano kati ya Iran na Russia inaongezwa muda wake

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, baadhi ya nyaraka na hati za mapatano kati ya Iran na Russia zinafuatiliwa na kwamba hati ya juu ya kuweka sawa uhusiano wa kistratejia kati ya nchi mbili ingalipo na sasa inaongezwa muda wake.

Akijibu swali mbele ya waandishi wa habari kuhusu uwezekano wa kusainiwa hati ya ushirikiano wa kistratejia kati ya Iran na Russia katika ziara ijayo ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Moscow, Saeed Khatibzadeh amesema kuwa: Safari hiyo itafanyika kufuatia mwaliko wa Rais Vladimir Putin.  

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameendelea kubainisha kuwa, ziara hiyo ni ya kikazi, na pande mbili zitajaribu kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali katika nyanja tofauti. 

Rais Vladimir Putin wa Russia amemwalika Rais Raisi mjini Moscow

Aidha akijibu swali kwamba siku kadhaa zilizopita kumekuwa na mijadala kuhusu kulegeza kamba Iran katika baadhi ya matakwa yake katika mazungumzo ya Vienna, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, kuwepo kwa matini iliyokubaliwa na pande mbili ni kielelezo kwamba, upande wa Magharibi umetambua kuwa unapaswa kulegeza kamba na kutupilia mbali matakwa yake ya juu na yaliyo  nje ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. 

Katika sehemu nyingine ya kikao chake na waandishi wa habari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Iran inasisitiza suala la kutimizwa matakwa ya wananchi huko Afghanstan na kuundwa serikali jumuishi.