China: Marekani ilitenda jinai ya kivita kwa kumuua Qasem Soleimani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema Marekanin ilitenda jinai ya kivita kwa kumuua Luteni Jenerali Qasem Soleimani, kamanda wa Iran aliyeongoza vita dhidi ya ugaidi.
Akizungumza Jumanne, Wang Wenbin amesema: "Mauaji ya Qasem Soleimani ni mfano mwingine wa namna Marekani inavyovuruga kiholela kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhusiano wa kimataifa. Ni moja kati ya jinai za kivita ambazo zimefanywa na Marekani." Amesema Marekani ilimuua kamanda wa kijeshi wa nchi huru kwa njia za kigaidi na huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Wang ametoa tamko hilo akijibu swali la mwandishi habari kuhusu maadhimisho ya mwaka wa pili tokea alipouawa Kamanda Soleimani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameongeza kuwa, Marekani pia imekuwa ikitekeleza jinai za kivita kote duniani kwa kuwaua malaki ya raia wasio na hatia. Ameongeza kuwa Marekani inafanya vitendo hivyo vilivyo kinyume cha sheria na jinai kote duniani nyuma ya pazia la madai yake ya inachokiita 'mfumo wa kimataifa wenye kuzingatia sheria."
Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambaye Januari 3 mwaka 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi vamizi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Hujuma hiyo ilitekelezwa kwa amri ya rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.
Kufuatia jinai hiyo, mnamo Januari 8 mwaka 2020, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilichukua hatua ya kulipiza kisasi kwa kuvurumisha makombora kadhaa dhidi ya kituo cha kijeshi cha Marekani cha Ain al Assad nchin Iraq.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa bado haijamaliza kulipiza kisasi mauaji ya Shahidi Soleimani na kwamba kuondoka askari wote wa Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia ndiko kutalipiza kisasi damu ya Luteni Jenerali Soleimani.