Sheikh Naim Qassem: Kamanda Soleimani ni shahidi wa Umma
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78852-sheikh_naim_qassem_kamanda_soleimani_ni_shahidi_wa_umma
Akizungumzia mafanikio ya Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, Kamanda Soleimani alikuwa shahidi wa Umma.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2022 04:15 UTC
  • Sheikh Naim Qassem: Kamanda Soleimani ni shahidi wa Umma

Akizungumzia mafanikio ya Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, Kamanda Soleimani alikuwa shahidi wa Umma.

Sheikh Naim Qassem ambaye Jumanne jioni alikuwa akizungumza kwa mnasaba wa kukumbuka mwaka wa pili wa kuuawa shahidi Kamanda Qasem Soleimani katika hafla iliyofanyika kwenye ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Beirut, alisema kuuliwa shahidi kwa kamanda huyo sio tu kwamba hakukupunguza nguvu na thamani za muqawama, lakini pia kuliinua juu ari na nafasi ya wanamapambano.

Amesisitiza kuwa Kamanda Soleimani alikwenda mbali zaidi ya nchi yake na kuwa shahidi wa Umma wa Kiislamu na kwamba hilo ni jambo lenye umuhimu mkubwa. 

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, Shahidi Qasem Soleimani alithabitisha dira ya mapambano ya ukombozi wa Palestina kwa kadiri kwamba, sasa hakuna mtu anayeweza kupotosha njia ya mapambano hayo. 

Luteni Jenerali Qasem Soleimani

Sheikh Naim Qassem amesema:"Ni haki ya makundi ya mapambano kushirikiana na wamiliki wa ardhi iliyoghusubiwa kwa ajili ya kukabiliana na kambi ya shari ya wale ambao wameamua kutuita sisi kuwa ni magaidi ilhali wao wenyewe ndio nembo kuu ya dhulma na mauaji ya halaiki duniani."

Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambaye Januari 3 mwaka 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi vamizi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Hujuma hiyo ilitekelezwa kwa amri ya rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.