Jenerali Hajizadeh: Iran itazindua 'kombora la kistratejia' karibuni
Kamanda wa Kikosi cha Anga na Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema karibuni hivi kikosi hicho cha SEPAH kitazindua kombora jipya la kistratejia katika uga wa mifumo ya ulinzi wa anga.
Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh alisema hayo jana Jumatatu katika hafla iliyofanyika kwa ajili ya kumuenzi Kiongozi mwandamapinduzi na muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini MA wakati huu ambapo taifa la Iran linaadhimisha mwaka wa 43 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Brigedia Jenerali Hajizadeh ameashiri mafanikio makubwa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika uga wa ulinzi hususan uzalishaji wa makombora na kueleza kuwa, "kombora hilo la kistratejia litazindulia katika mustakabali wa karibu."
Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la SEPAH ameeleza bayana kuwa, Iran imepiga hatua kubwa ya kujitosheleza katika uga wa ulinzi, na hii ni stratejia ya ushindi iliyochukuliwa na Iran dhidi ya madola ya kibeberu.
Hivi karibuni, Iran ilizindua kombora jipya la balestiki la baharini lililoundwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) liitwalo Zulfiqar, lenye uwezo wa kulenga shabaha chini ya bahari iliyoko umbali wa kilomita 700.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo kubwa wa makombora ya balestiki unaowatia kiwewe maadui wa taifa hili. Hivi karibuni, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilikiri kuwa, Iran ina uwezo mkubwa wa makombora zaidi ya taifa lolote lile la Asia Magharibi.